Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika inapita kwa
mbinde katika kikao cha Bunge la bajeti 2013 mjini Dodoma hivi karibuni.
Taarifa zinabainisha kwamba haikuwa rahisi kupita
kwa bajeti hiyo kutokana na sababu nyingi, lakini kubwa ni mfumo wa
stakabadhi ghalani na utaratibu wa ruzuku ya pembejeo, ushirika na
sintofahamu iliyopo kwa wakulima wa pamba, miwa na tumbaku.
Mazao hayo ingawa ni roho ya uchumi wa mataifa
mengi ulimwenguni, nchini wakulima wake wapo njia panda na mbaya zaidi
hata fedha zizozotengwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kilimo
hazieleweki zinaenda wapi na zinafanya nini?
Hata hivyo bajeti ya serikali 2012/2013
haijaonyesha kutoa nafuu yoyote kwa wenye viwanda vidogo na wakulima na
hali hiyo kuwaweka njiapanda watendaji katika sekta hizo kwani
kilichotokea katika bajeti iliyopita haikuakisi nuru kwa bajeti ijayo.
Kulingana na Waziri wa Fedha na Uchumi, William
Mgimwa, Sh17.7 trilioni, zimetengwa kwa ajili ya bajeti ya mwaka
2012/2013 na bajeti ya sasa inatenga fedha za matumizi makubwa katika
mafungu matano.
Mafungu hayo ni pamoja na kulipa deni la Taifa
ambalo limetengewa Sh2.7 trilioni wakati Wizara ya Ujenzi Sh1 trilioni,
ulinzi Sh920 bilioni, elimu Sh721 Bilioni na nishati na madini Sh641
bilioni. Jumla ya fedha zote ambazo zitatumika kama mafungu ya juu ni
Sh5.982 Trilioni.
Serikali katika bajeti ijayo katika kile
ilichoelezwa kuwa ni kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa mikopo
ya muda mrefu, kilimo kisichokuwa na tija na ukosefu wa ajira, imetenga
fedha katika maeneo tofauti kwa ajili ya la kuhuisha sekta ya kilimo.
Kulingana na bajeti ya sasa, Sh30 bilioni
zimetengwa kwa ajili ya Benki ya Rasilimali (TIB) Sh40 bilioni kwa Benki
ya Maendeleo ya Kilimo, fedha ambazo zinaifanya benki hiyo mpya kuwa na
mtaji wa Sh100 bilioni.
Waziri Mgimwa anasema bajeti imelenga kuboresha mazingira ya biashara na kutenga maeneo maalum ya uwekezaji mijini na vijijini.
Anasema lengo lingine ni kukuza ubia kati ya sekta
ya umma na sekta binafsi na hatua hiyo inaenda sanjari na kuboresha
viwanda vidogo vidogo nchini na kwamba Sh128.4 bilioni, zimetengwa
katika eneo hilo.
Bajeti ya serikali katika sekta ya kilimo inatajwa
Sh328.1 bilioni kwa ajili ya maendeleo ya kilimo, na Sh130.5 bilioni
kwa ajili ya ruzuku ya pembejeo na Sh5.7 kwa ajili ya ushirika ambao
unalalamikiwa kuwa ni kama umekufa.
No comments:
Post a Comment