Friday, June 7, 2013

Wakulima 940,800 wafaidi mbolea ya ruzuku

Katika mwaka wa fedha 2012/13, Serikali ilitoa ruzuku ya tani 126,117 za mbolea ambapo jumla ya wakulima 940,783 walinufaika na tani 8,278 za mbegu bora za mahindi huku wakipata mbegu bora za mpunga tani 1,694.

Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Waziri wa Kilimo,Chakula na Ushirika Christopher Chiza ambaye alisema kuwa mipango hiyo imetokana na kukubalika kwa baadhi ya mazao ya chakula kuruhusiwa na kuwa mazao ya biashara.

Alikuwa akijibu swali la Martha Mosesi Mlata (Viti Maalumu-CCM), ambaye alitaka kujua kama Serikali inatambua kwamba kuna baadhi ya mazao ambayo ni chakula lakini yanatumika kama mazao ya biashara hivyo kuna sababu ya kuyapa ruzuku.

Mlata alihoji pia sababu za wakulima wa Mkoa wa Singida kuzuiwa wasilime zao la mahindi licha ya kuwa zao hilo linastawi vizuri mkoani humo.

Waziri alisema Serikali ilijikita katika kutoa mbolea ya ruzuku na pembejeo ili kuboresha uzalishaji wa mazao hayo na kuhakikisha wakulima wanapata chakula cha kutosha na kuwaongezea kipato.

Alisema kuanzia mwaka 2013/14 hadi 2015/16, Wizara kupitia mfumo wa matokeo makubwa imejiwekea malengo ya kuongeza uzalishaji kwa kiasi cha mahindi tani 100,000 na mchele tani 290,000 katika mashamba mapya ya wakulima wakubwa na wadogo.

Kwa mujibu Chiza, katika miradi hiyo Serikali inatarajia kutumia Sh 91.5 bilioni kugharimia ruzuku ya pembejeo za mazao zikiwamo mbolea.

Thursday, June 6, 2013

Teknolojia kuandaa miche ; Mbinu mpya ya kuongeza uzalishaji wa korosho

Wakulima wakitumia teknolojia ya kisasa kubebesha mikorosho katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo Naliendele mkoani Mtwara hivi karibuni.

Wednesday, June 5, 2013

Wafugaji, wawindaji nchini waridhishwa Rasimu Katiba

Arusha
Mtandao wa Jamii za pembezoni za Wafugaji, Wawindaji wa Asili na Waokota Matunda, umeeleza kuridhishwa na rasimu ya Katiba Mpya iliyotambua uwapo wao na kulindwa rasilimali na tamaduni wao.
Mratibu wa Taasisi ya Katiba-Initiative iliyoundwa na mashirika yanayotetea jamii hizo, William Ole Nasha alisema mapendekezo yao mengi yamechukuliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Kimsingi tumeridhishwa na rasimu hii, maombi yetu mengi yameingizwa na sasa haki za jamii hizi, ambazo ni ndogondogo zitalindwa,” alisema Ole Nasha.
Pia, alisema haki za wafugaji ambao wamekuwa wakikabiliwa na matatizo mengi zimeingizwa na kwamba, sehemu nyingi ya rasimu itakuwa ikijulikana kuwa Tanzania kuna wakulima, wafugaji na wavuvi.
“Siyo kutambuliwa tu bali mifugo imetambuliwa kama zao la uchumi la wafugaji, pia ni maisha na mila,” alisema Ole Nasha.
Naye Mwanasheria wa Mtandao wa Mashirika ya Wafugaji wa Asili na Waokota Matunda (Pingo’s Forum), Emmanuel Saringe alisema wanaunga mkono rasimu hiyo, lakini walitaka wafugaji kuondolewa kwenye kundi dogo katika jamii.
“Wafugaji ni wengi hasa hawa wa asili, tungependa watajwe kama kundi kubwa ambalo linahitaji kutambulika ingawa kwa sasa linatajwa katika rasimu kama sehemu ya makundi madogomadogo,” alisema Saringe.
Alisema wafugaji ni kundi kubwa katika jamii, ambalo lipo nyuma kwa maendeleo, hivyo linapaswa kupewa kipaumbele na katiba.
“Wafugaji ni kundi maalumu, hivyo linapaswa kulindwa katika katiba na kuendelezwa kwani lipo nyuma,” alisema Saringe.

Tuesday, June 4, 2013

Wakulima miwa wataka kulipwa fidia ya hasara


Mvomero. 
Serikali imeshauriwa kuwalipa fidia wakulima wa miwa waliopata hasara na umaskini wa kipato kutokana na soko la miwa lisilo na tija.
Soko hilo linadaiwa kuwafanya wakulima hao kushindwa kuendelea na kilimo hicho, kinachoonekana kukosa msisimko wilayani Mvomero, mkoani Morogoro.
Akizungumza kwenye mkutano wa wanachama, Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Wakulima wa Miwa na Mazao Mengine Turiani (Tucopricos) Wilaya ya Mvomero, Majaliwa Kayanda alisema sheria zinazohusu miwa zinaonekana kumbeba zaidi mwekezaji na kumsahau mkulima mdogo.
Kayanda alishauri Serikali kufanyia kazi haraka mapendekezo yaliyofikiwa kwenye kikao na wakulima, kilichoitishwa na Wizara ya Viwanda na Biashara Machi mwaka huu.
Katika kikao hicho viwanda vinavyonunua miwa ya wakulima nchini vilihudhuria na kukubaliana na kwamba, kila mkulima anafahamu kiwango cha sukari kinachotoka katika muwa wake kabla ya kupelekwa kiwandani. Kwa upande wao, wakulima wa chama hicho walibainisha kuwapo kwa changamoto mbalimbali zinazohitajika kutatuliwa ili kumnusuru mkulima.
Changamoto hizo ni wafugaji kuvamia mashamba, huku Serikali ikishauriwa kuruhusu kuwapo kiwanda kingine cha sukari kuweka ushindani wa bei, badala ya soko kuhodhiwa na kiwanda kimoja.