Friday, May 17, 2013

Wakulima wanusurika kifo

WAKULIMA wawili wilayani Kiteto, wamenusurika kuuawa na wafugaji jamii ya Kimasai baada ya kuibuka mapigano kufuatia ng’ombe kula mazao shambani.
Wakulima hao walionusurika kuuawa ni Samweli Malima (35) na Sanagali Athumani (29), wote wakazi wa Njutaa.
Akizungumza na Mwakilishi wa Blog Yetu jana hospitalini walipolazwa majeruhi, baba mzazi wa majeruhi hao, Waziri Mtambo (55) alisema tukio hilo lilitokea Mei 15, majira ya saa 7 mchana wakati vijana hao wakiwa shambani wakivuna mahindi.
Alisema vijana hao walipofika shambani waliwakuta ng’ombe wanakula mazao ndipo walipowauliza vijana wachungaji waliokuwa wakichunga ng’ombe hao na ndipo ukatokea ubishani.
Mtambo alisema baada ya muda mfupi walitokea Wamasai sita kwenye kibanda cha shambani ambacho Malima na Athumani kipindi hicho walikuwa wamepumzika na kuomba na wao kupumzika wakidai wamechoka baada ya kutembea umbali mrefu wakichunga ng’ombe ambao hawakuwa nao.
“Baada ya muda wakaongezeka tena Wamasai wengine na kuanza kuwachoma choma na sime ubavuni huku wakihoji kwanini wanazuia ng’ombe wasile chakula,” aliongeza.Alisema kutokana na hali hiyo, vijana hao walianza kujitetea, lakini walizidiwa nguvu na Athumani alizimia ndipo walipokimbia.
Mtambo alisema vijana hao waliokolewa na wapita njia ambao walitoa taarifa kijijini na wananchi kwenda mashambani ambako waliwakuta wametapakaa damu huku wakiwa wamepoteza baadhi ya viungo vya mwili.
“Athumani ambaye hali yake ni mbaya amechanwa na sime kichwani na kupasua mfupa wa fuvu, ametobolewa kwapani na sime, paji la uso kushoto karibu na jicho, amechunwa ngozi hadi usawa wa sikio na sime na Samweli Malima amekatwa dole gumba la mkono wa kulia, amejeruhiwa kichwani kwa sime na sehemu mbalimbali mwilini,” alifafanua.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa alikiri kuwepo kwa tukio hilo na kwamba tayari askari wameagizwa kwenda kudhibiti hali katika eneo hilo.

Thursday, May 16, 2013

Sh4 bilioni zatumika kwa kilimo Rukwa

Katika Kipindi cha mwaka wa fedha 2007/08 hadi 2010/11, Serikali imetoa Sh4 bilioni kwa ajili ya kusaidia miradi ya umwagiliaji katika Mkoa wa Rukwa , Bunge liliambiwa jana.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima ambaye alisema kuwa fedha hizo zilipelekwa katika maeneo ya Sakalilo, Katuka, Singiwe, Maleza, Ulumi, Ng’ongo na Lwafi/ Katongo.
Malima alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Abia Nyabakari (Viti Maalumu-CCM) ambaye alihoji ni kwa nini Serikali isione umuhimu wa kuupa kipaumbele Mkoa wa Rukwa katika masuala ya kilimo cha umwagiliaji.
Naibu Waziri alisema kuwa Serikali imekuwa ikiupa kipaumbele Mkoa wa Rukwa kutokana na ukweli kuwa unazalisha mazao mengi ya kutosheleza mkoa na kutoa ziada kwa mikoa mingine na ghala la Taifa.
Alisema katika kipindi hicho pia Serikali ilitoa ruzuku ya pembejeo za kilimo, mbolea na mbegu bora na kwamba jumla ya kaya 546,647 zilipata ruzuku hiyo hiyo pamoja na mbegu bora za mahindi bila matatizo.

Serikali yaahidi kugawa mbegu bora kwa wakulima nchini

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika imeweka mkakati madhubuti wa kuwapatia wakulima mbegu na mbolea kwa utaratibu ulio bora na wenye maslahi mapana, Bunge lilielezwa jana.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima ambaye alisema kuwa mkakati huo utatokana na ushauri wa kitaalamu wa kutoka kwa watalaamu wa ngazi zote wakiwamo wakulima, watafiti, wagani na mawakala wa mbolea.
Alikuwa akijibu swali la Athuman Mfutakamba (Igalula-CCM) aliyehoji juu ya Serikali kuwapatia wakulima wa maeneo ya Uyui mbegu bora na kuwabadilishia kutoka mbegu za zamani na kuwapatia mbegu za mahindi aina ya DKC 8053.
Malima alisema kuwa utaratibu uliopo ni kwa wakulima wa halmashauri husika kuwasilisha wizarani mahitaji halisi ya aina ya mbegu za mahindi wanazopendelea.
Kuhusu utaratibu wa utoaji wa ruzuku ya pembejeo kwa utaratibu wa vocha, alisema wakulima hunufaika kwa kupatiwa seti ya vocha tatu za mbolea ya kupandia.
Mbali na mbegu za mahindi lakini alisema wakulima kwa baadhi ya maeneo hupewa mbegu bora za mpunga ambapo wakulima wa eneo husika huchagua mbegu wanayoihitaji baada ya kushauriwa na maofisa ugani.

Monday, May 13, 2013

Zao la korosho kuendelea kuzama kwa sera mbovu

 

Dar es Salaam. Imeelezwa kwamba wakulima wa Korosho nchini wataendelea kupata mapato duni hadi hapo Serikali itakaposaidia uwekezaji wa viwanda vya ubanguaji wa korosho katika mikoa inayolima zao hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti ya Kuondoa Umaskini (Repoa), Profesa Samwel Wangwe alisema juzi kwamba uuzaji wa korosho zisizobanguliwa nje ya nchi ni hasara kwa wakulima.
Profesa Wangwe alisema hayo wakati wa majadiliano ya utafiti unaolinganisha ufanisi wa zao hilo kati ya Tanzania na Vietnam uliofanywa na Dk Blandina Kilama wa Repoa.
“Tunahitaji kuongeza thamani ya zao hili kwa kujenga viwanda vya kisasa vya kubangua korosho  ili tuweze kuuza kwa thamani itatayowanufaisha wakulima,” alisema Profesa Wangwe.
Wakati Profesa Wangwe akisema hayo, viwanda vya kubangua korosho ambavyo Serikali ilibinafsisha kwa watu binafsi, vimegeuzwa maghala ya kuhifadhia mazao na kusababisha korosho kuuzwa zikiwa hazijabanguliwa.
Kwa upande wake, Dk Kilama alisema katika utafiti wake kwamba ingawa Tanzania ilianza kilimo cha korosho kabla ya Vietnam lakini nchi hiyo iko juu kiuzalishaji kuishinda Tanzania.
Alisema kinachowasaidia ni kwamba mbali na Serikali hiyo kuweka sera bora za kilimo, pia kuna viwanda vingi vya kubangua korosho hali inayowafanya waongeze thamani ya zao hilo.
“Hata Bodi ya Korosho ya Vietnam inajumuisha wataalamu wa kilimo, wakulima na wabanguaji jambo ambalo ni tofauti hapa kwetu ambapo bodi inaweza kuwa na watu ambao siyo wadau wa korosho,” alisema na kuongeza kwamba Tanzania imeshuka kwa kiasi cha kutisha katika uzalishaji zao


Mwenyekiti wa wakulima kizimbani, anunua pamba bila leseni

Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima wa Pamba Tanzania (Tacoga), Elias Zizi amepandishwa kizimbani kwa kosa la kuhujumu kilimo cha zao.
Zizi anashtakiwa kwa kununua pamba kabla ya msimu, ikiwamo kufanya biashara ya pamba bila leseni.
Mwendesha Mashtaka Polisi, Clement Kitundu alidaiwa mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alikamatwa May 6, mwaka huu Kijiji cha Mbiti, Kata ya Mango, wilayani Bariadi, akinunua pamba.
Kitundu alidai kuwa suala hilo ni kosa tena bila leseni. Ilidaiwa kuwa kwa vipindi na siku tofauti, mshtakiwa ambaye ni kiongozi wa chama cha wakulima anayetambua na kuelewa sheria na kanuni, alitenda kosa hilo na kufanikiwa kununua zaidi ya tani moja ya pamba kwa nia ya kuiuza baadaye.
Mshtakiwa alikana mashtaka hayo na kuachiwa kwa dhamana, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Bariadi, Robert Oguda aliamua mahakama kuhamia eneo la tukio kupima na kushuhudia pamba hiyo ikiwamo kupima uzito, kazi iliyofanyika chini ya usimamizi wa polisi.