Thursday, May 16, 2013

Serikali yaahidi kugawa mbegu bora kwa wakulima nchini

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika imeweka mkakati madhubuti wa kuwapatia wakulima mbegu na mbolea kwa utaratibu ulio bora na wenye maslahi mapana, Bunge lilielezwa jana.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima ambaye alisema kuwa mkakati huo utatokana na ushauri wa kitaalamu wa kutoka kwa watalaamu wa ngazi zote wakiwamo wakulima, watafiti, wagani na mawakala wa mbolea.
Alikuwa akijibu swali la Athuman Mfutakamba (Igalula-CCM) aliyehoji juu ya Serikali kuwapatia wakulima wa maeneo ya Uyui mbegu bora na kuwabadilishia kutoka mbegu za zamani na kuwapatia mbegu za mahindi aina ya DKC 8053.
Malima alisema kuwa utaratibu uliopo ni kwa wakulima wa halmashauri husika kuwasilisha wizarani mahitaji halisi ya aina ya mbegu za mahindi wanazopendelea.
Kuhusu utaratibu wa utoaji wa ruzuku ya pembejeo kwa utaratibu wa vocha, alisema wakulima hunufaika kwa kupatiwa seti ya vocha tatu za mbolea ya kupandia.
Mbali na mbegu za mahindi lakini alisema wakulima kwa baadhi ya maeneo hupewa mbegu bora za mpunga ambapo wakulima wa eneo husika huchagua mbegu wanayoihitaji baada ya kushauriwa na maofisa ugani.

No comments:

Post a Comment