Thursday, February 27, 2014

MSITU WA RUVU KUSINI KIBAHA HATARINI KUTOWEKA




Msitu wa Ruvu Kusini uliopo wilayani Kibaha, Mkoa wa Pwani upo hatarini kutoweka baada ya kuvamiwa na wananchi wanaofanya shughuli zao ndani ya eneo la msitu huo zikiwemo zile za ukataji miti, uchomaji mikaa na ujenzi wa mabwawa ya samaki.

Kutokana na hatari hiyo, wananchi wa maeneo hayo wameiomba Serikali kusimamisha shughuli zinazofanywa katikati ya msitu huo kwa kuwa hatua hiyo inaweza kusababisha kutoweka kwa msitu huo.
Mbali na hilo, wananchi wa vijiji vya Boko Mnemera na Mpiji vilivyopo jirani na mashamba hayo wamekitupia lawama Kitengo cha Mitambo na Mizani kilichopo chini ya Wakala wa Barabara nchini (Tanrods) kuruhusu mitambo yao kuingia na kufanya uchimbaji wa mabwawa katika mashamba hayo.

Wakizungumza na waandishi wa habari waliotembelea maeneo hayo, wananchi wa maeneo hayo waliiomba Serikali kuingilia kati uvamizi wa maeneo hayo na kutafuta suluhu haraka ili kuepusha hatari ya ukame inayowanyemelea.Mwenyekiti wa Kijiji cha Mpiji na Boko Mnemera, Said Mwenyegoha, ameiomba Serikali kuingilia kati vitendo hivyo.
 
Alisema miongoni mwa waliovamia katika msiku huo wameanzisha uchimbaji wa mabwawa ya samaki hatua anayosema haikufuata taratibu za kupata kibali kutoka Serikali ya kijiji na kuufunga mkondo wa maji unaotegemewa na wanakijiji hao.Mwenyegoha anasema tayari wametoa taarifa ofisi za wilaya kuhusiana na uharibifu unaofanywa na wavamizi hao.

 Hadi sasa hakuna hatua za haraka zilizochukuliwa.Wamiliki wa shamba la mifugo la Soga na Alavi Estate, lililoko maeneo ya jirani na msitu huo wa Serikali wanasema hatua iliyofanywa na wavamizi ya kuingia katika maeneo ya mashamba na misitu hiyo italeta athari kubwa kwa wanavijiji wa maeneo hayo.

Mmiliki wa Soga Faisal Edha, anasema mashamba hayo pamoja na msitu yamekuwa na faida kubwa kwa Taifa kutokana na kuzalisha maziwa lita 2,000 kila siku pamoja na kuzalisha mitamba na kusambaza kwa wananchi maeneo mbalimbali nchini.

Alionya, endapo Serikali itashindwa kufunga mabwawa hayo kuna uwezekano wa kutoweka kwa mashamba hayo pamoja na misitu huku wananchi wa vijiji hivyo wakiwa hatarini kukosa maji.
“Tunaomba Serikali ichukue hatua haraka maana iwapo wavamizi hawa wataachwa na hasa huyu aliyechimba mabwawa kuna uwezekano wa mifugo yetu kufa kutokana na ukame,” alisema.

Naye Meneja wa Mashamba ya Alavi Estate, Amir Mndeme anasema suala hilo lina athari kubwa kwa wanavijiji hivyo Serikali haipaswi kulinyamazia jambo hilo bali lichukue hatua za haraka ili kunusuru mashamba hayo kuendelea kutoa uzalishaji.



Akizungumzia suala la mtambo wa Tanroad kuhusika katika uchimbaji wa mabwawa hayo, Mkuu wa Kitengo cha Mitambo na Mizani wa wakala huyo, Sylvester Semfukwe anasema kuwa mtambo huo ulikodishwa Februari 14, mwaka huu na mtu mmoja (jina linahifadhiwa) na kwamba mamlaka hiyo haikujua mtambo unaenda wapi na kufanya shughuli gani.

Anasema Kitengo cha Biashara cha mamlaka hiyo kimekuwa kikikodisha mitambo yake kwa wananchi na mashirika bila kuhoji shughuli zinazoenda kufanywa na kuitaja gharama ya ukodishaji wa mtambo huo kwa saa nane kuwa ni Sh650,000 ambazo zililipwa na mteja aliyekodi mitambo hiyo.
 


WAJASIRIAMALI WAPATA MAFUNZO USINDIKAJI MUHOGO




WAJASIRIAMALI 16 kutoka Mikoa ya Mwanza, Pwani na Kagera wamepata elimu ya usindikaji wa zao la muhogo na viwango vinavyozingatia ubora unaokubalika katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EA C).

Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, wilayani Misungwi baada ya mafunzo hayo, mshauri wa usindikaji na masoko wa IITA Dkt. Gabriel Nduguru, alisema wakulima wasindikaji wa zao la muhogo, hawakuwa na elimu ya kutosha kuhusu viwango na ubora wa bidhaa zao.

 Alisema kuwa mafunzo hayo kwa wasindikaji hao, yalitolewa na Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo Alisema wanafanya utafiti wa mazao na kusaidia kuainisha viwango vinavyotumika kwa nchi za EAC, baada ya kuridhiwa na mawaziri wa nchi za Jumuiya hiyo.

Alisema wananchi watafahamu viwango vya ubora baada ya kuwapa mafunzo ya usindikaji na watazalisha chakula chenye ubora na kuuza katika masoko ya uhakika na watajiongezea kipato .

cha Kitropiki (IITA) kwa kushirikiana na Shirika la Viwango nchini (TBS ).
Alisema IITA ilifanya utafiti na kubaini changamoto hiyo kwa wasindikaji wengi wa zao la muhogo, hivyo ikaamua kutoa elimu inayohusu ubora na viwango kwa wasindikaji hao ili kuwawezesha kupata masoko ya uhakika.

"Wakulima na wasindikaji hao hawakuwa na elimu, hivyo bidhaa zao hazikuwa bora na salama na zilitishia afya za walaji.Baada ya kubaini hilo tukaona tuwafundishe jinsi ya kusindika muhogo salama kwa kuzingatia viwango vya ubora kulingana na mahitaji ya walaji," alisema Dkt. Ndunguru.

Dkt. Ndunguru alisema changamoto kubwa kwa wasindikaji zao la muhogo, ni vifungashio na mitambo ya kisasa kwani ni kiwanda kimoja tu ambacho hakitoshelezi mahitaji.
 


Wednesday, February 26, 2014

USIMAMIZI HAFIFU WACHANGIA SAMAKI KUPOTEA MKOANI MARA


 

IMEELEZWA kuwa usimamizi hafifu wa kanuni na sheria za uvuvi ndani ya Ziwa Victoria ndio chanzo kinachochangia kupotea kwa samaki mkoani Mara. Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Mfawidhi ulinzi na rasilimali za uvuvi Mkoa wa Mara, Braison Meela wakati akitoa taarifa katika kikao cha wadau wa uvuvi katika ziwa hilo kilichofanyika kwenye ukumbi wa uwekezaji uliopo katika Ofisi ya mkuu wa mkoa huo.

Meela alisema kuwa kumekuwepo na wasimamizi wabovu katika kusimamia kanuni na sheria ya uvuvi kuanzia ngazi ya kata hadi Taifa hali inayochangia kupungua kwa rasilimali hiyo ambayo ndiyo inayoingiza pato kubwa katika nchi hii .

Alisema kuwa lengo ni kuchukua hatua stahiki ili kuwa na rasilimali endelevu ya samaki katika ziwa hilo litakalofikiwa iwapo hatua sahihi na za makusudi zitachukuliwa dhidi ya wanaosababisha kupungua wingi wa samaki hao ndani ya ziwa.

Akizungumzia kuhusu changamoto zilizopo katika sekta hiyo alisema kuwa ongezeko la matumizi ya mbinu haramu ya uvuvi kama vile matumizi ya dawa za kilimo ya kuvulia samaki, usimamizi hafifu wa sheria na kanuni zake kama vile wataalam, BMU, wanasiasa na serikali ya vijiji ambapo matokeo yanaachwa yanaenda kama yalivyo ikiwa ni pamoja na ukosefu wa maadili na ukiukwaji wa miiko ya utumishi kwa baadhi ya watendaji.

"Nyavu za timba ni nyavu ambazo zimekuwa zikitumiwa mara kwa mara kuvulia samaki kwa njia ya uvuvi haramu na nyavu hizi zinatokea nchi za nje kwani wanaozingiiza ni wenzetu kwa kuwa wanajua bidhaa hiyo ina soko hapa kwetu hivyo tunapaswa kila mmoja kuwa mlinzi wa rasilimali hii," alisema Meela.

Akizungumzia viashiria vya kupungua kwa samaki alisema kuwa viwanda vya samaki vinazalisha kwa kiwango cha chini ya asilimia hamsini ya uwezo wake, hivyo kushindwa kukidhi mahitaji ya wateja wao.
Mmoja wa wadau hao ambaye ni mwenyekiti wa Halmashauri ya Butiama Magina Magesa alisema kuwa inashangaza sana kuona hapa nchini hakuna viwanda vinavyozalisha nyavu hizo, lakini nyavu hizo zimezagaa katika maeneo mbalimbali ndani ya nchi huku vyombo vya dola vimeshindwa kudhibiti uingizwaji wa nyavu hizo.

Mkuu wa Mkoa wa Mara John Tuppa akifungua kikao hicho alisema kuwa BMU ambao ndio kama ya kufuatilia matumizi mabaya ya zana hizo lakini hao ndio wanaowakingia kifua wavuvi haramu kwa kuwaambia wafiche zana hizo wakati wa oparesheni ili wakimaliza waendelee na shughuli zao kama kawaida.

Alisema nchi jirani zinazozungukwa na ziwa hilo wananufaika na mazao ya ziwa hilo lakini Mkoa wa Mara umeshindwa kunufaika na mazao yanayotokana na ziwa hilo kwa sababu ya watu wa BMU kutokuwa na maadili ya utendaji kazi kama dhamana yao.