Msitu wa Ruvu Kusini uliopo wilayani Kibaha, Mkoa wa Pwani upo hatarini kutoweka baada ya kuvamiwa na wananchi wanaofanya shughuli zao ndani ya eneo la msitu huo zikiwemo zile za ukataji miti, uchomaji mikaa na ujenzi wa mabwawa ya samaki.
Kutokana na hatari hiyo, wananchi wa maeneo hayo wameiomba Serikali kusimamisha shughuli zinazofanywa katikati ya msitu huo kwa kuwa hatua hiyo inaweza kusababisha kutoweka kwa msitu huo.
Mbali na hilo, wananchi wa vijiji vya Boko Mnemera na Mpiji vilivyopo jirani na mashamba hayo wamekitupia lawama Kitengo cha Mitambo na Mizani kilichopo chini ya Wakala wa Barabara nchini (Tanrods) kuruhusu mitambo yao kuingia na kufanya uchimbaji wa mabwawa katika mashamba hayo.
Wakizungumza na waandishi wa habari waliotembelea maeneo hayo, wananchi wa maeneo hayo waliiomba Serikali kuingilia kati uvamizi wa maeneo hayo na kutafuta suluhu haraka ili kuepusha hatari ya ukame inayowanyemelea.Mwenyekiti wa Kijiji cha Mpiji na Boko Mnemera, Said Mwenyegoha, ameiomba Serikali kuingilia kati vitendo hivyo.
Alisema miongoni mwa waliovamia katika msiku huo wameanzisha uchimbaji wa mabwawa ya samaki hatua anayosema haikufuata taratibu za kupata kibali kutoka Serikali ya kijiji na kuufunga mkondo wa maji unaotegemewa na wanakijiji hao.Mwenyegoha anasema tayari wametoa taarifa ofisi za wilaya kuhusiana na uharibifu unaofanywa na wavamizi hao.
Hadi sasa hakuna hatua za haraka zilizochukuliwa.Wamiliki wa shamba la mifugo la Soga na Alavi Estate, lililoko maeneo ya jirani na msitu huo wa Serikali wanasema hatua iliyofanywa na wavamizi ya kuingia katika maeneo ya mashamba na misitu hiyo italeta athari kubwa kwa wanavijiji wa maeneo hayo.
Mmiliki wa Soga Faisal Edha, anasema mashamba hayo pamoja na msitu yamekuwa na faida kubwa kwa Taifa kutokana na kuzalisha maziwa lita 2,000 kila siku pamoja na kuzalisha mitamba na kusambaza kwa wananchi maeneo mbalimbali nchini.
Alionya, endapo Serikali itashindwa kufunga mabwawa hayo kuna uwezekano wa kutoweka kwa mashamba hayo pamoja na misitu huku wananchi wa vijiji hivyo wakiwa hatarini kukosa maji.
“Tunaomba Serikali ichukue hatua haraka maana iwapo wavamizi hawa wataachwa na hasa huyu aliyechimba mabwawa kuna uwezekano wa mifugo yetu kufa kutokana na ukame,” alisema.
Naye Meneja wa Mashamba ya Alavi Estate, Amir Mndeme anasema suala hilo lina athari kubwa kwa wanavijiji hivyo Serikali haipaswi kulinyamazia jambo hilo bali lichukue hatua za haraka ili kunusuru mashamba hayo kuendelea kutoa uzalishaji.
Akizungumzia suala la mtambo wa Tanroad kuhusika katika uchimbaji wa mabwawa hayo, Mkuu wa Kitengo cha Mitambo na Mizani wa wakala huyo, Sylvester Semfukwe anasema kuwa mtambo huo ulikodishwa Februari 14, mwaka huu na mtu mmoja (jina linahifadhiwa) na kwamba mamlaka hiyo haikujua mtambo unaenda wapi na kufanya shughuli gani.
Anasema Kitengo cha Biashara cha mamlaka hiyo kimekuwa kikikodisha mitambo yake kwa wananchi na mashirika bila kuhoji shughuli zinazoenda kufanywa na kuitaja gharama ya ukodishaji wa mtambo huo kwa saa nane kuwa ni Sh650,000 ambazo zililipwa na mteja aliyekodi mitambo hiyo.
No comments:
Post a Comment