Tuesday, February 25, 2014

WAKULIMA WA TUMBAKU KUNUFAIKA







WAKULIMA wa zao la tumbaku mkoani Tabora watanufaika na ongezeko la bei ya zao hilo huku pembejeo zake zikishuka bei kwa kiwango kikubwa.

Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa Bodi ya muda ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU), Hassan Wakasuvi alipozungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kurejea kutoka nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu ya mguu.
Wakasuvi alisema kwa muda mfupi ambao Bodi hiyo imekuwepo madarakani imefanikiwa kufanya mambo mengi likiwemo kusimamia na kuhakikisha wakulima wananufaika na zao hilo kwa kuuza kwa bei yenye tija.

Alisema kuwa katika msimu wa kilimo wa mwaka 2012/2013 mbolea aina ya NPK iliuzwa kwa dola 53.90 ambapo msimu wa mwaka 2013/2014 iliuzwa kwa dola 51.35 ikiwa na tofauti ya dola 2.55.
Aidha alisema kuwa mbolea aina ya CAN katika msimu wa 2012/2013 iliuzwa kwa dola 38.60 ambapo msimu wa2013/2014 iliuzwa kwa 33.30 ikiwa na tofauti ya dola 5.30.

Aliendelea kufafanua kuwa mbolea aina ya UREA katika msimu wa kilimo wa 2012/2013 iliuzwa kwa dola 46.60 na msimu wa mwaka 2013/2014 kuuzwa kwa dola 34.85 sawa na tofauti ya dola 11.75.
Pia alisema Confidor ya pakiti katika msimu wa mwaka 2013/2014 iliuzwa kwa dola 4.46 ambapo katika msimu wa 2013/2014 iliuzwa kwa dola 2.88 ikiwa na tofauti ya dola 1.58.

Alisema dawa aina ya Yavikonyo katika msimu wa 2012/2013 iliuzwa kwa dola 28.94 na 2013/2014 ikiuzwa kwa dola 20.60 sawa na tofauti ya dola 8.34.

Wakasuvi alisema katika kipindi hicho cha bodi ya muda pia walifanikiwa kuokoa fedha kiasi cha dola za Marekani 236,088.72 sawa na Sh 4,632,844,632 kutokana na tofauti ya bei ya msimu wa kilimo katika mwaka 2012/2013 na 2013/2014.

No comments:

Post a Comment