USIMAMIZI HAFIFU WACHANGIA SAMAKI KUPOTEA MKOANI MARA
IMEELEZWA kuwa usimamizi hafifu wa kanuni na
sheria za uvuvi ndani ya Ziwa Victoria ndio chanzo kinachochangia kupotea kwa
samaki mkoani Mara. Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Mfawidhi ulinzi na rasilimali
za uvuvi Mkoa wa Mara, Braison Meela wakati akitoa taarifa katika kikao cha
wadau wa uvuvi katika ziwa hilo kilichofanyika kwenye ukumbi wa uwekezaji
uliopo katika Ofisi ya mkuu wa mkoa huo.
Meela alisema kuwa kumekuwepo na wasimamizi
wabovu katika kusimamia kanuni na sheria ya uvuvi kuanzia ngazi ya kata hadi
Taifa hali inayochangia kupungua kwa rasilimali hiyo ambayo ndiyo inayoingiza
pato kubwa katika nchi hii .
Alisema kuwa lengo ni kuchukua hatua stahiki
ili kuwa na rasilimali endelevu ya samaki katika ziwa hilo litakalofikiwa iwapo
hatua sahihi na za makusudi zitachukuliwa dhidi ya wanaosababisha kupungua
wingi wa samaki hao ndani ya ziwa.
Akizungumzia kuhusu changamoto zilizopo
katika sekta hiyo alisema kuwa ongezeko la matumizi ya mbinu haramu ya uvuvi
kama vile matumizi ya dawa za kilimo ya kuvulia samaki, usimamizi hafifu wa
sheria na kanuni zake kama vile wataalam, BMU, wanasiasa na serikali ya vijiji
ambapo matokeo yanaachwa yanaenda kama yalivyo ikiwa ni pamoja na ukosefu wa
maadili na ukiukwaji wa miiko ya utumishi kwa baadhi ya watendaji.
"Nyavu za timba ni nyavu ambazo zimekuwa
zikitumiwa mara kwa mara kuvulia samaki kwa njia ya uvuvi haramu na nyavu hizi
zinatokea nchi za nje kwani wanaozingiiza ni wenzetu kwa kuwa wanajua bidhaa
hiyo ina soko hapa kwetu hivyo tunapaswa kila mmoja kuwa mlinzi wa rasilimali
hii," alisema Meela.
Akizungumzia viashiria vya kupungua kwa
samaki alisema kuwa viwanda vya samaki vinazalisha kwa kiwango cha chini ya asilimia
hamsini ya uwezo wake, hivyo kushindwa kukidhi mahitaji ya wateja wao.
Mmoja wa wadau hao ambaye ni mwenyekiti wa Halmashauri ya Butiama Magina Magesa
alisema kuwa inashangaza sana kuona hapa nchini hakuna viwanda vinavyozalisha
nyavu hizo, lakini nyavu hizo zimezagaa katika maeneo mbalimbali ndani ya nchi
huku vyombo vya dola vimeshindwa kudhibiti uingizwaji wa nyavu hizo.
Mkuu wa Mkoa wa Mara John Tuppa akifungua
kikao hicho alisema kuwa BMU ambao ndio kama ya kufuatilia matumizi mabaya ya
zana hizo lakini hao ndio wanaowakingia kifua wavuvi haramu kwa kuwaambia
wafiche zana hizo wakati wa oparesheni ili wakimaliza waendelee na shughuli zao
kama kawaida.
Alisema nchi jirani zinazozungukwa na ziwa
hilo wananufaika na mazao ya ziwa hilo lakini Mkoa wa Mara umeshindwa kunufaika
na mazao yanayotokana na ziwa hilo kwa sababu ya watu wa BMU kutokuwa na
maadili ya utendaji kazi kama dhamana yao.
No comments:
Post a Comment