MAHIZA AWAKUNA WAKULIMA WA KOROSHO
WAKULIMA
wa zao la korosho mkoani Pwani wamefurahishwa na uamuzi wa Mkuu wa mkoa huo, Mwantumu
Mahiza kutaka maofisa ushirika kuwajibishwa kwa kuwaondoa maofisa ushirika
kutokana na utendaji mbovu na kushindwa kufuatilia madeni ya mikopo kwa vyama
vya ushirika na fedha za wakulima wa zao la korosho.
Mahiza alitoa agizo hilo kwenye kikao cha ushauri cha mkoa (RCC) kilichofanyika
hivi karibuni mjini Kibaha na kubainisha kuwa ni kipindi kirefu aliomba matokeo
ya kulipwa kwa madeni ya mikopo hiyo na fedha za wakulima hao suala ambalo
usimamizi wake umeonekana sio wa kuridhisha.
Mkuu huyo wa mkoa alitaka kuwajibishwa kwa watendaji hao kutokana na vyama vya
ushirika wa mazao (AMCOS) vilivyofanya biashara kwa kutumia mfumo wa stakabadhi
za mazao ghalani msimu wa 2011/2012 kwa kutumia fedha kwa kukusanya mazao ya
wakulima ambazo zilipatikana kutokana na mikopo toka kwenye taasisi za kibenki
za NMB na CRDB ambapo jumla ya sh. bil 12 zilikopwa.
Mmoja wa wakulima wa zao hilo la korosho wilayani Kibaha, Peter Malundi alisema
watendaji hao hawana msaada wowote hali ambayo inasababisha shughuli za kilimo
cha zao hilo kutokuwa na manufaa kutokana na fedha zao nyingi kutolipwa kwa
walikopwa korosho zao muda mrefu.
Malundi alisema kuwa hata deni hilo kubwa ambalo lilikopwa benki hizo kwa
udhamini wa mkoa lingeweza kulipwa endapo watendaji hao wangekuwa makini lakini
kutokana na kutowajibika ipasavyo kumechangia hali hiyo.
"Kauli ya Mahiza kusema kuwa kwasasa hawataki watendaji hao ambao hawana
manufaa na mkoa huo hususan wakulima hivyo haina budi kupitia kikao hicho
kutamka rasmi hawafukuzi bali hawataki mkoani hapo kwa maslahi ya mkoa ni kauli
inayoonyesha uwajibikaji na iwe fundisho kwa watendaji wengine," alisema
Malundi.
Alisema kuwa baadhi ya watendaji ndani ya mkoa huo wamekuwa hawawajibiki na
kuona kuwa Mkoa wa Pwani ni sehemu ya kupumzika pasipo kufanya kazi jambo hilo
si sahihi kwani na wananchi wa mkoa huo nao wanataka maendeleo kama ilivyo
mikoa mingine.
"Kwa kuwa mkuu wa mkoa alisema kuwa mwanzo wa mkakati wake wa mwaka 2014
kutaka uwajibikaji kwa watendaji kwenda kwa wananchi na kusimamia kero zilizopo
pasipo kukaa kusubiri kero mezani kutoka kwa wananchi ni mpango mzuri,"
alisema Malundi.
Awali hatua iliyochukuliwa na Serikali kupitia wizara ya kilimo na ushirika
iliwataka viongozi na watendaji wa vyama vya msingi kulipa madeni yaliyotokana
na uzembe wao sambamba na kuwaondoa viongozi hao na kuteua bodi mpya.
No comments:
Post a Comment