WAKULIMA WA PAMBA WAMLALAMIKIA RC
CHAMA cha Wakulima wa Pamba nchini (TACOGA) kimemlalamikia Mkuu wa Mkoa
wa Geita, Magalula Said Magalula, kwa kitendo chake cha kuagiza kukamatwa na
kuwekwa ndani kwa wawekezaji watatu wa zao la pamba akiwatuhumu kushindwa
kufunga mikataba na wakulima .
Kwa mujibu wa tamko lililotolewa kwa waandishi wa habari juzi mjini Kahama
mkoani Shinyanga na mwenyekiti wa TACOGA, Elias Zizi, kitendo cha hicho
kinadaiwa kupingana na agizo lililotolewa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete,
alipoagiza wakulima wasilazimishwe kujiunga na mpango wa kilimo cha mkataba
mpaka pale watakapokuwa wamepewa elimu ya kutosha.
Zizi aliwataja wawekezaji waliokamatwa na kuwekwa ndani kwa agizo la mkuu huyo
wa mkoa kuwa ni pamoja na mwakilishi wa kampuni ya Fresho Investment, Kampuni
ya ICK Cotton Co. Ltd na Kahama Oil Mill Ltd ambao wote wanafanya shughuli zao
katika mkoa huo wa Geita.
Mwenyekiti huyo ameelezea kushangazwa kwake na hatua ya mkuu wa mkoa huo ambayo
amedai ni matumizi mabaya ya madaraka aliyopewa na Rais Kikwete na kwamba
mpango wa kilimo cha mkataba pamoja na kuwa ni hiari hata hivyo baada ya
majaribio yake kulijitokeza changamoto kadhaa katika utekelezaji wake.
Akifafanua, alisema baada ya kujitokeza kwa changamoto hizo wadau wote
walikubaliana kusitishwa kwa muda utekelezwaji wa mpango huo mpaka pale
changamoto zilizojitokeza zitakapopatiwa utatuzi ikiwemo suala la elimu duni
juu ya mpango huo kutobainishwa vizuri kuhusu faida au hasara zake.
Kutooneshwa wazi kwa bei ya pamba atakayolipwa mkulima pale atakapokuwa anauza
pamba yake licha ya kukopeshwa huduma zote muhimu ambazo bei zake zinafahamika
pamoja na kilimo hicho kutokuwa na bima itakayomlinda mkulima iwapo patatokea
janga lolote kama vile suala la ukame.
"Lakini changamoto nyingine ni suala la vikundi vya wakulima kutosajiliwa
kisheria hali inayowanyima haki ya kudai na kudaiwa kisheria, uwekezaji mdogo
wa mkopeshaji ukilinganisha na jasho la mkulima wa pamba analowekeza kwa eneo
moja.
"Sisi TACOGA tunalaani kitendo cha Mkuu wa Mkoa wa Geita kwa hatua ya
kutoa agizo la kukamatwa kwa wawekezaji hao katika zao la pamba ambapo wanatoa
huduma katika mkoa wake, kitendo hicho kimelenga kuzishinikiza pande mbili
pasipo hiari yao kuingia kwenye kilimo hicho cha mkataba."
Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita, Magalula, pamoja na kukiri kutoa agizo la kukamatwa
na kuwekwa ndani kwa wawekezaji hao alikanusha sababu zilizotolewa na viongozi
wa TACOGA na kufafanua kuwa kosa lao ni lakuwauzia wakulima viuatilifu kwa
fedha taslimu badala ya kuwapa kwa mkopo kama yalivyo maelekezo ya Bodi ya
pamba (TCB).
"Nikweli nilitoa agizo wakamatwe, lakini hao TACOGA wanapotosha ukweli,
sijawakamata kwa kutokuwa na vikundi vya kilimo cha mkataba, bali ni kutokana
na kukiuka kwao utaratibu wa usambazaji dawa hizo za kuua wadudu ambapo mbali
ya kuuza kwa fedha taslimu fedha hizo hawakuziwasilisha bodi ya pamba ambayo
ndiyo iliyowapatia dawa hizo," alieleza Magalula.
No comments:
Post a Comment