Tuesday, February 25, 2014

ZAO LA MIWA LIINGIZWE KATIKA MFUMO WA PEMBEJEO ZA KILIMO


ZAO LA MIWA

 

UMOJA wa Wakulima wa Kilimo cha Miwa mkoani Kagera (KASGA) wameiomba serikali kuliingiza zao la miwa
katika mfumo wa pembejeo za kilimo ili kupunguza gharama za kununua dawa ambazo ni kubwa na 
kuwasababishia kushindwa kumudu.

Mmoja wa wakulima hao, Anasi Swaibu alibainisha hayo hivi karibuni mjini Kyaka wakati akizungumza
na mwandishi wa habari hizi juu ya changamoto zinazowakabili katika kilimo hicho.Swaibu alisema sasa wakati
umefika Serikali kuliingiza zao hilo katika mfumo wa pembejeo ili kuondoa ukiritimba ambao upo kwa sasa katika
maduka ya wauzaji binafsi wa dawa au pembejeo zinazotumika katika kilimo hicho.

Alisema mfano dawa ya kuulia magugu ambayo huuzwa zaidi ya Sh 16,000 kwa lita moja hapa Tanzania wakati
nchini Uganda dawa hiyo hiyo huuzwa kwa gharama ya Sh 10,000 jambo ambalo linasababisha wakulima hao 
kushindwa kulima kilimo chenye tija kilicho bora.

Gharama hiyo ni kubwa kwa mkulima wa kawaida kama sisi itakuwa vigumu kuendelea, basi Serikali ilione hili la
kuweka zao hili katika mfumo wa pembejeo kama yalivyo mazao kama korosho maana tunajikuta asilimi 90 ya
faida hiyo inaishia katika ununuzi wa dawa,”alihoji Swaib.

Mkulima mwingine wa miwa, Ahmed Kajubi alishauri kama Serikali haiwezi kuweka utaratibu wa pembejeo za
ruzuku katika zao hilo basi viwanda vya sukari nchini viweke utaratibu wa jinsi ya kukopesha pembejeo kwa 
wakulima hao pale wakipeleka miwa waweze kurejesha au kuwauzia wakulima wadogo pembejeo hizo kwa bei ya
kawaida ili waweze kumudu gharama hizo na kufanya kilimo cha miwa kuwa cha uhakika na kupendwa na 
wakulima wengi.


No comments:

Post a Comment