Wednesday, February 26, 2014

WAKULIMA NCHINI WATAKIWA KUTUMIA MAOFISA UGANI




WAKULIMA nchini wameshauriwa kuwatumia maofisa ugani wa Kata kwa ajili ya kupata ushauri kuhusu kilimo cha kitaalamu ili wajipatie mavuno mengi kulingana na shamba walilolima.

Ushauri huo ulitolewa juzi na Ofisa Masoko wa Kampuni ya Kuuza Mbegu za Nafaka (SEED.CO) mkoani Morogoro, Silas Ngowe, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mkoani hapa. Alishauri wakulima wa Mkoa wa Morogoro kupanda mbegu za muda mfupi kutokana na mvua kupungua ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Mbali na ushauri huo, Ngowe aliwataka wakulima kuwafanya maofisa ugani kama waganga wao kwa kuwapatia ushauri na kwamba wasiwapuuze kwa sababu ndiyo msaada wao."Kwa kawaida mgonjwa anapoumwa hukimbilia kumtafuta daktari hivyo na hawa wakulima nawashauri wawe wanawatafuta mara kwa mara maofisa ugani kwa ajili ya maelezo ya mashamba yao," alisema Ngowe .

Kuhusu pembejeo za vocha, alisisitiza kuwa wakulima wachukue mbegu na mbolea kwenye maduka waliyopangiwa na Serikali. Kuhusu tatizo la wakulima kuuza vocha zao ameshauri wasiziuze badala yake wazitumie kama Serikali ilivyoagiza na kwamba mkulima ambaye hana shida na vocha hizo awaachie wenye shida na si kuuza kwa bei nafuu.

"Unakuta mkulima anapata vocha kwa bei nafuu halafu anaamua kuuza kwa bei ya chini kitu ambacho si sahihi, ni vizuri kama mkulima huyo hahitaji vocha awaachie wakulima wanaohitaji na si kuuza kwa bei rahisi," alisema. Ngowe alisisitiza wakulima kuchukua kiwango kilichoandikwa kwenye vocha kiwe ndicho kiwango mwafaka na si vinginevyo .

No comments:

Post a Comment