Katika Kipindi cha mwaka wa fedha 2007/08 hadi 2010/11, Serikali
imetoa Sh4 bilioni kwa ajili ya kusaidia miradi ya umwagiliaji katika
Mkoa wa Rukwa , Bunge liliambiwa jana.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Waziri wa
Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima ambaye alisema kuwa fedha hizo
zilipelekwa katika maeneo ya Sakalilo, Katuka, Singiwe, Maleza, Ulumi,
Ng’ongo na Lwafi/ Katongo.
Malima alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la
Abia Nyabakari (Viti Maalumu-CCM) ambaye alihoji ni kwa nini Serikali
isione umuhimu wa kuupa kipaumbele Mkoa wa Rukwa katika masuala ya
kilimo cha umwagiliaji.
Naibu Waziri alisema kuwa Serikali imekuwa ikiupa
kipaumbele Mkoa wa Rukwa kutokana na ukweli kuwa unazalisha mazao mengi
ya kutosheleza mkoa na kutoa ziada kwa mikoa mingine na ghala la Taifa.
Alisema katika kipindi hicho pia Serikali ilitoa
ruzuku ya pembejeo za kilimo, mbolea na mbegu bora na kwamba jumla ya
kaya 546,647 zilipata ruzuku hiyo hiyo pamoja na mbegu bora za mahindi
bila matatizo.
No comments:
Post a Comment