Tuesday, June 4, 2013

Wakulima miwa wataka kulipwa fidia ya hasara


Mvomero. 
Serikali imeshauriwa kuwalipa fidia wakulima wa miwa waliopata hasara na umaskini wa kipato kutokana na soko la miwa lisilo na tija.
Soko hilo linadaiwa kuwafanya wakulima hao kushindwa kuendelea na kilimo hicho, kinachoonekana kukosa msisimko wilayani Mvomero, mkoani Morogoro.
Akizungumza kwenye mkutano wa wanachama, Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Wakulima wa Miwa na Mazao Mengine Turiani (Tucopricos) Wilaya ya Mvomero, Majaliwa Kayanda alisema sheria zinazohusu miwa zinaonekana kumbeba zaidi mwekezaji na kumsahau mkulima mdogo.
Kayanda alishauri Serikali kufanyia kazi haraka mapendekezo yaliyofikiwa kwenye kikao na wakulima, kilichoitishwa na Wizara ya Viwanda na Biashara Machi mwaka huu.
Katika kikao hicho viwanda vinavyonunua miwa ya wakulima nchini vilihudhuria na kukubaliana na kwamba, kila mkulima anafahamu kiwango cha sukari kinachotoka katika muwa wake kabla ya kupelekwa kiwandani. Kwa upande wao, wakulima wa chama hicho walibainisha kuwapo kwa changamoto mbalimbali zinazohitajika kutatuliwa ili kumnusuru mkulima.
Changamoto hizo ni wafugaji kuvamia mashamba, huku Serikali ikishauriwa kuruhusu kuwapo kiwanda kingine cha sukari kuweka ushindani wa bei, badala ya soko kuhodhiwa na kiwanda kimoja.

No comments:

Post a Comment