Morogoro. Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika, Christopher Chiza amesema kuwa Tanzania inatarajia kuzalisha
tani 80,000 za kahawa ifikapo mwaka 2016 nia ikiwa ni kuongeza
uzalishaji wa zao hilo na kukidhi masoko ya ndani na nje ya nchi.
Chiza pia alisema kuwa Tanzania imekuwa ikizalisha
wastani wa tani 35,000 na 50,000 za aina mbalimbali za kahawa kwa mwaka
ikiwa ni pamoja na aina ya Arabica, Robusta zenye soko kubwa katika
soko la dunia.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa wadau wa
kahawa unaofanyika mjini Morogoro, Waziri Chiza alisema wizara yake
imeweka mikakati mbalimbali ya kuboresha zao hilo ikiwa ni pamoja na
kuongeza mikoa minane ya ulimaji wa zao hilo ambayo ni pamoja na
Morogoro, Iringa, Njombe, Katavi, Geita na Manyara huku Serikali
ikiendelea kujenga mazingira mazuri zaidi ya kilimo cha zao hilo.
Alisema hakuna sababu ya kilimo cha zao hilo
kushuka, kwa kuwa zao hilo lina bei nzuri katika soko la dunia,
akiwataka Watanzania kuzalisha kwa wingi hata pale bei ya zao hilo
inaposhuka katika soko la dunia kwa kuwa imekuwa na mtindo wa kupanda na
kushuka mara kwa mara.
“Zao la kahawa ni muhimu sana na ni lazima kuwapo
na utaratibu wa kuwa na bei moja yenye manufaa kwa mkulima na nchi yetu
kwani mkulima amekuwa na mahitaji makubwa ya kimaisha na anatakiwa
kukuza uchumi wake,” alisema waziri huyo.
Waziri Chiiza alisema, umefika wakati wa kuanza
kutafuta masoko mapya ndani na nje ya nchi badala ya kung’ang’ania soko
moja na kujikita katika kulalamika na kuongeza kuwa ili kuweza
kufanikiwa katika kutafuta masoko hayo, ni lazima balozi zitumike
kusaidia ili wakulima waweze kunufaika.
Alisema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau
na bodi ya kahawa kusaidia kupitia ruzuku kila mwaka na kuzitaka
halmashauri kutenga maeneo ya kilimo cha kahawa na kuweka bustani za
miche ya zao hilo ili wakulima waweze kupata miche hiyo kwa bei nafuu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mkutano huo, Seleman
Chambo mapema akimkaribisha Waziri Chiza alisema kuwa, uzalishaji wa
zao la kahawa nchini umeshuka kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni
pamoja na baadhi ya mashamba ya kahawa kulimwa mazao mengine huko mkoani
Kilimanjaro wakati baadhi ya wadau wa kahawa nchini wakilalamikia
kutofuatwa kwa bei elekezi ya kahawa.
No comments:
Post a Comment