Thursday, May 30, 2013

Stakabadhi ghalani yaongeza gharama kwa wakulima


Utaratibu ulioanzishwa na serikali wa kuuza bidhaa za mkulima kwa mfumo wa stakabadhi ghalani (WRS) katika baadhi ya maeneo yenye uzalishaji mkubwa, umeelezwa kuongeza gharama kwa mkulima, licha ya kuwapo kwa faida katika mfumo huo.
Kitendo cha wakulima kulipa tozo kwa kilo moja ya mazao inayonunuliwa kwa mfumo huo ni mzigo mzito kwa wakulima. Utafiti mpya unaonyesha kwamba
dawa ya kuondokana na gharama hizo ni wakulima kujiunga katika ushirika na kujiendesha wenyewe.
Imeelezwa kwamba ushirika huo utawasaidia wakulima kutumia vyema fursa za kiuchumi katika kuzalisha, kuhifadhi na kupata soko la uhakika.
Tunalipa Sh2 milioni
Ofisa Mtendaji wa Taasisi ya RUDI ambayo kazi yake ni kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini, Abel Lyimo akizungumzia utafiti mpya unaohusu mfumo wa stakabadhi ghalani unaojulikana ‘Tanzania Warehouse Legal Framework and its Impact on Sesame and Rice Farmers,’amesema wakulima wanalazimika kumwajiri Meneja Dhamana wa kushughulikia mfumo huo na kwamba wanamlipa Sh2 milioni kwa mwezi.

Lyimo anasema utafiti huo uliangalia athari za
kisheria na kiutendaji wa mfumo wa stakabadhi ghalani kwa mazao ya ufuta na mpunga.
“Hii ni gharama kubwa kwa wakulima, kwanini wamwajiri Meneja Dhamana wa kuangalia ghala?” anahoji Lyimo. Anafikiri kwamba ni vyema wakulima
waachwe wachague namna nzuri ya kuhifadhi na kuuza bidhaa zao kupitia ushirika.
Kwa mujibu wa utafiti huo kitendo cha kumwajiri Meneja Dhamana ni kigumu kwa kuwa wataalamu wa aina hiyo wana gharama kubwa na inakuwa ngumu zaidi wanapotaka kulipwa kwa dola za Marekani, yaani fedha za kigeni.
Kwa mtazamo mwingine endapo wakulima wanapatiwa mafunzo na kwa kuzingatia teknolojia ya asili, wanaweza kabisa kuhifadhi mazao yao ghalani tena kwa ufanisi zaidi kuliko Meneja Dhamana.
“Mameneja dhamana wengi  hawana uzoefu na mazingira ya eneo husika,” anasema Lyimo. Anasema kupitia vyama vya ushirika gharama nyingi zisizokuwa na maana zitapungua kwa upande wa wakulima.
Kwa mujibu wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Mpunga cha Kilombero(AKIGIRO), shughuli ya hifadhi na masoko wao wanafanya vyema.
Kwa mujibu wa taarifa ya utafiti huo kuna tatizo la  maghala hivi sasa na yaliyopo yanaonekana kutumika kibinafsi zaidi,
na kusababisha wakulima kutokuwa na uwezo wa kudhibiti. Wakati mwingine wakulima wanalazimishwa kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani hata kama
hawautaki mfumo huo.
Pia imebainika kwamba ni vigumu kwa wakulima kuteta na bodi yenye dhamana na masuala ya maghala kutokana na kuwapo kwa urasimu.
Kwa mujibu wa utafiti huo, wakulima hasa wale wa ufuta wa Mkoa wa Lindi wamekuwa katika mgogoro na serikali ya mkoa kwa sababu serikali hiyo iliwataka wauze ufuta kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani na si vinginevyo.
Wakulima wa mpunga wa Kilombero wamesema bodi ya stakabadhi ghalani katika  eneo lao imekuwa na sheria kali ikiwa ni pamoja na kuwazuia wakulima wadogo kujenga na kumiliki maghala yao.
“Kwa mfano ili ghala litambulike katika mfumo wa malipo ya stakabadhi ghalani iwe na uwezo wa kuchukua si chini ya tani 200 na masharti mengine ambayo ni magumu,” inasema taarifa hiyo.


Kanuni zilizowekwa zinawazua watu binafsi na wakulima wadogo na wale
wa makundi kumiliki maghala yao katika maeneo yao,”inasema sehemu ya taarifa ya utafiti huo.
Kwa mujibu wa utafiti huo Halmashauri ya Kilwa mwaka 2012/13 iliamua
kujitoa katika mfumo wa Stakabadhi ghalani baada ya kubaini
kwamba wanapoteza fedha nyingi kwa kukumbatia mfumo huo.
“Sababu kubwa ni kwamba bei iliyokuwa inatolewa na chama cha ushirika
cha ILULU ilikuwa ndogo kuliko zile zinazotolewa katika mikoa ya Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani zinazopakana na wilaya ya Kilwa,” inasema
taarifa hiyo.
Kuhakikisha kwamba mkulima, vyama vya msingi na serikali za mitaa zinafaidika, halmashauri ilitengeneza muundo mwingine wa soko la ufuta na pia mfumo wa soko la wazi ulidhibitiwa. Imeelezwa kwamba faida kubwa ya mfumo huo katika Wilaya ya Kilwa, gharama nyingi zilizopo katika mfumo wa stakabadhi ghalani, ziliondolewa.
“Wafanyabiashara walielekezwa kwenda katika vijiji kadhaa, kuamsha ushindani wa kibiashara,bei ya juu ilipatikana na hivyo kuongeza kipato kwa mkulima, vyama vya ushirika vya msingi na kwenye serikali za mitaa,” inasema taarifa hiyo iliyodhaminiwa na BEST AC.

Taarifa ya utafiti huo inaonyesha kwamba tofauti na mifumo mingine na  gharama za usafirishaji zinamezwa na mkulima. Katika mfumo huo mnunuzi
anabeba gharama za usafirishaji kwa kiwango kikubwa.
Mnunuzi alikuwa ananunua gunia la kuhifadhia mazao na kulipia riba za benki.

Kutokana na mfumo huo Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa iliingiza kama kodi katika mfuko wake Sh395 milioni katika msimu wa mwaka 2012/2013 kutoka Sh70 milioni katika miaka iliyopita,huku vyama vya msingi vikiwa vimevikusanya Sh250 milioni  na Sh7 bilioni.
Kwa upande wake mwanzilishi wa shirikisho la wakulima waliohitimu vyuo vikuu Stephano Kingazi anasema wakulima hawana nongwa na mfumo wa stakabadhi ghalani, lakini hawataki serikali kuwalazimisha kuuza au kutouza mazao yao.
“Wakulima wengi wanakubaliana na ukweli kwamba mfumo wa stakabadhi ghalani ni mzuri kwao, lakini wanasema kuna makato mengi kwa kilo
na kusababisha mzigo mzito kwa mkulima,” anasema Dk Kinganzi katika mahojiano hivi karibuni mkoani Morogoro.

Kwa mujibu wa utafiti huo, wakulima wa mpunga walikuwa wanakatwa asilimia
15 katika Wilaya ya Kilombero katika mfumo wa stakabadhi ghalani, asilimia 29 wilayani Lindi na asilimia 8 Kilwa kutokana na mfumo wake.
Wakulima wawe huru
“Kinachoonekana hapa, kuna watu wengi wanachukua fedha kwa mkulima hata kabla mazao yake hayajafikia mwisho wa safari.
“Itakuwa vyema kama wakulima watafanya shughuli za kuuza mazao yao
bila kuingiliwa na mtu,” inasema taarifa ya utafiti huo.
Kwa mujibu wa utafiti, stakabadhi ghalani inakuwa na faida zaidi kwa wakazi wa vijijini. Dk Elibariki Msuya, miongoni mwa watu walioandaa taarifa ya utafiti huo amesaema ingawa Tanzania inasheria nzuri zinazowezesha mfumo wa
stakabadhi ghalani ukilinganisha na majirani zake, bado serikali haijaufikisha mfumo huo mahali pa zuri.

“Wadau mbalimbali wameonyesha matatizo hapa na pale katika mifumo tofauti inayofanyakazi nchini kwa lengo la kusaidia wakulima; mfumo wa Mkoa wa Lindi unaonekana kuwa kikwazo,kwani una sheria nyingi zinazobana katika soko la wazi na unaonekana ni dhaifu.
Katika mfumo wa Kilwa unaonekana kuwa na nafuu zaidi na mzuri kwa wakulima kwani ulifanikiwa kupunguza tozo mbalimbali,” anabainisha Dk Msuya.
Mfumo wa Kilombero unawezesha mfumo wa stakabadhi ghalani kufanyakazi huku pia watu binafsi wakiendelea kufanyakazi na kumpa fursa mkulima kuchagua soko lenye bei nzuri.
 Habari zaidi:
Kuna maghala 60 katika mikoa 19.
Biashara ya maghala nchini inasimamiwa na Bodi ya kutoa leseni ya Maghala ambayo inafanyakazi chini ya sheria namba 10 ya mwaka 2005 ya stakabadhi ghalani na kanuni zake za mwaka 2006.
 Tangu kuanzishwa kwa bodi hiyo imetoa leseni kwa maghala 60 katika mikoa 19 yenye uwezo wa kuhifadhi tani 267,000.

No comments:

Post a Comment