Friday, June 7, 2013

Wakulima 940,800 wafaidi mbolea ya ruzuku

Katika mwaka wa fedha 2012/13, Serikali ilitoa ruzuku ya tani 126,117 za mbolea ambapo jumla ya wakulima 940,783 walinufaika na tani 8,278 za mbegu bora za mahindi huku wakipata mbegu bora za mpunga tani 1,694.

Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Waziri wa Kilimo,Chakula na Ushirika Christopher Chiza ambaye alisema kuwa mipango hiyo imetokana na kukubalika kwa baadhi ya mazao ya chakula kuruhusiwa na kuwa mazao ya biashara.

Alikuwa akijibu swali la Martha Mosesi Mlata (Viti Maalumu-CCM), ambaye alitaka kujua kama Serikali inatambua kwamba kuna baadhi ya mazao ambayo ni chakula lakini yanatumika kama mazao ya biashara hivyo kuna sababu ya kuyapa ruzuku.

Mlata alihoji pia sababu za wakulima wa Mkoa wa Singida kuzuiwa wasilime zao la mahindi licha ya kuwa zao hilo linastawi vizuri mkoani humo.

Waziri alisema Serikali ilijikita katika kutoa mbolea ya ruzuku na pembejeo ili kuboresha uzalishaji wa mazao hayo na kuhakikisha wakulima wanapata chakula cha kutosha na kuwaongezea kipato.

Alisema kuanzia mwaka 2013/14 hadi 2015/16, Wizara kupitia mfumo wa matokeo makubwa imejiwekea malengo ya kuongeza uzalishaji kwa kiasi cha mahindi tani 100,000 na mchele tani 290,000 katika mashamba mapya ya wakulima wakubwa na wadogo.

Kwa mujibu Chiza, katika miradi hiyo Serikali inatarajia kutumia Sh 91.5 bilioni kugharimia ruzuku ya pembejeo za mazao zikiwamo mbolea.

No comments:

Post a Comment