Wednesday, November 7, 2012

Bei mpya ya korosho yatangazwa



Bodi ya Korosho Tanzania imetangaza bei ya kununulia korosho kwa msimu wa 2012/ 2013 kwa wakulima.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa bodi hiyo. Mudhihir Mudhihiri, alisema katika msimu huo kilo moja ya korosho kwa daraja la kwanza itakuwa inanunuliwa kwa Sh. 1200 wakati daraja la pili itanunuliwa kwa Sh. 960 kwa kilo.
Mudhihili alisema kwamba wadau wa korosho wamekubaliana kuwa wakulima watalipwa malipo yao kwa awamu mbili na malipo ya kwanza yatakuwa asilimia 70 ya bei dira na ya pili yatakuwa asilimia 30.
Aliongeza kuwa kwa mwaka huu zoezi la kukusanya korosho kwa wakulima ambalo hufanywa na vyama vya msingi kwa katika msimu wa manunuzi limechelewa kufanyika kutokana na vyama hivyo kuchelewa kupata mikopo ya kuviwezesha kulipia zao hilo kwa wakulima.
Mudhihili alisema licha ya msimu wa ununuzi wa zao hilo kufunguliwa tangu Septemba mwaka huu, lakini ununuzi huo umechelewa kuanza na hivyo kuwaathiri sana wakulima.
Aliongeza kuwa akutokana na tatizo hilo, Waziri wa Chakula, Ushirika na Masoko, Christopher Chiza, aliamua kuitisha kikao cha dharura kilichojumuisha Bodi ya Korosho, Bodi ya Leseni ya Maghala, Wizara ya Viwanda na Biashara, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Benki ya CRDB, NMB na Benki ya Rasilimali (TIB) kwa ajili ya kuzungumzia mkanganyiko wa bei dira.

No comments:

Post a Comment