Nimepanda karoti lakini sitaki
kutumia dawa za viwandani kuua magugu mbali na kupalilia kwa mikono ni
dawa gani za asili ninazoweza kutumia kuua magugu?
Magugu ni tatizo kubwa kwa karoti. Hii ni kwa sababu ni zao linalokuwa taratibu na pia majani yake si mapana kuweza kuweka kivuli halikadhalika kupambana na wadudu. Magugu yasipodhibitiwa, yataathiri mavuno kwa kiasi kikubwa. Kwa bahati mbaya hakuna dawa za asili za kuulia magugu. Viini vyovyote vinavyoweza kutumika kuulia magugu ni wazi kuwa pia vinaweza kuathiri mazao pia. Hivyo, wakulima wanaofanya kilimo hai hufanya palizi kwa kutumia mikono au mashine.
Utunzaji wa karoti kwa njia ya kilimo hai, ni lazima uanze hata kabla ya wakati wa palizi. Panda karoti sehemu ambayo haina magugu mengi, na ambayo haija athiriwa sana na magugu kama vile mbaruku, mtunguja na nyasi. Panda karoti kwenye sehemu uliyovuna mazao kama vile maboga, matango, tikiti, vitunguu au spinachi. Baada ya kuvuna mazao yaliyotangulia, lima shamba lako na upande mbegu za karoti kwenye kitalu kisichokuwa na magugu.
Udongo ni lazima uvunjwe vizuri ili kuepusha hali itakayozuia mizizi kwenda chini ipasavyo. Karoti inahitaji udongo unaoweza kuruhusu kwenda chini vizuri, na unaopitisha maji vizuri, na wenye kiasi kikubwa cha malighafi zinazo oza (udongo mweusi). Utunzaji wa udongo kwa ajili ya kilimo hai, ni pamoja na kuweka mbolea vunde, pamoja na matandazo ambayo huongeza rutuba kwenye udongo kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo wakati wa kupanda karoti, inabidi shamba lisiwe na mabaki ya mazao ambayo hayaozi kwa kuwa yanaweza kuathiri uotaji wa mbegu za karoti. Endapo dawa za kuulia magugu zitatumika, inabidi zitumike kabla ya kupanda kwa kuwa zinaweza kuuwa miche ya karoti pia.
Karoti zinahitaji kukua kwa haraka bila vipingamizi ili kuwa na majani pamoja na mizizi iliyo imara. Kupalilia mapema ni muhimu ili kuepuka upotevu wa mavuno, hasa katika wiki 10 za mwanzo toka kuota. Wakulima wa karoti hutumia jembe la mkono kupalilia kati ya mstari na mstari wa miche ya karoti. Lakini magugu yanayo ota katikati ya karoti ni lazima yang’olewe kwa mikono. Kuwa makini ili usijeruhi mimea! Kwa kawaida kupalilia kwa kutumia jembe la mkono hufanyika mara 3 katika kipindi chote cha ukuaji.
No comments:
Post a Comment