Monday, November 26, 2012

Wakulima watakiwa kuchangamkia fursa

WAZIRI wa Kilimo na Chakula, Injinia Christopher Chiza, amewataka wakulima na wafanyabiashara nchini kuchangamkia fursa mbalimbali zinazojitokeza katika sekta hiyo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo wakati akiwaaga wakulima kutoka mikoa nane ya Tanzania Bara ambao wanakwenda Sudan kwa ajili ya maonyesho ya kilimo na warsha, Chiza alisema wakulima wengi wanatabia ya kuuza mazao yakiwa shambani, hali inayowafanya wasiendelee kimaisha.
Alisema katika maonesho hayo ya siku tano anatarajia wakulima watanufaika na mpango huo ikiwemo kukuza biashara ya kilimo na kupata fursa mbalimbali zinazohusiana na masuala ya kilimo.
Chiza alisema kuwa wakulima wanatakiwa wawe wajanja, kwani kwasasa watu wanaotoka nchi za nje wamekuwa wakisajili magari yao kwa namba za Tanzania ili wapate urahisi wa kusafirisha mazao wanayoyachukua nchini.
Naye mmoja wa wakulima hao, William Mbogo, alisema wanatarajia kupata soko, uzoefu utakaowaongezea tija katika kuzalisha mazao na kuonyesha bidhaa zao katika maonyesho hayo.
Jumla ya wakulima 11 kutoka Mikoa ya Iringa, Morogoro, Kilimanjaro, Katavi, Kagera, Arusha , Kigoma na Dodoma wanaondoka leo wakiambatana na Katibu Mkuu, Athuman Mfutakamba na Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Betty Mkwasa.

1 comment:

  1. Ni jambo la busara watanzania wakajifunza kwa bidii kilimo, kwani kwa kufanya hivyo itatuwezesha kuwa na chakula cha kutosha na kufanya shugliza maendeleo. Hivyo basi shime wadau wa kilimu kwa pamoja twaweza kwanda mbele.

    ReplyDelete