Thursday, November 29, 2012

Watanzania wahakikishiwa kutoporwa ardhi na wawekezaji

SERIKALI imewahakikishia Watanzania kwamba hakuna ardhi ya wanavijiji itakayochukuliwa kutoka kwao na kukabidhiwa wawekezaji kwa ajili ya miradi mikubwa ya kilimo.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Chrostopher Chiza, alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na wanavijiji toka vijiji vya Kidunda, Mkurazi na Usungura katika Wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani.
Waziri Chiza alikuwa ameambatana na kundi la wawekezaji waliokwenda kuangalia eneo la hekari 63,000 lililotengwa kwa ajili ya kilimo cha mpunga na miwa katika eneo la Gwata mkoani hapa. Ziara hiyo ilikuwa ni moja ya ratiba ya mkutano mkubwa wa wawekezaji wa kilimo uliofanyika jijini Dar es Salaam.
“Kunyang’anya ardhi wananchi sio sera yetu hata kidogo. Hizo ni propaganda zinazoenezwa na baadhi ya watu kwa nia mbaya,” alisema.
Alisema sera ya serikali ni kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha maisha ya Watanzania yanainuka na si vinginevyo na kwamba serikali imetayarisha mpango mzuri wa matumizi bora ya ardhi kwa maslahi ya nchi.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwapo na madai kutoka taasisi na watu mbalimbali wanaodai maelfu ya ardhi ya wakazi asilia katika maeneo mbalimbali Afrika yanaporwa na kuuziwa au kukodishwa kwa wawekezaji wakubwa na hata serikali za nje ya bara hilo.
Mapema katika mkutano huo uliotayarishwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na kituo cha mpango maalum wa uendelezaji kilimo katika ukanda wa kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisisitiza wawekezaji wote katika ukanda wa SAGCOT kupewa kipaumbele pale ambapo uwekezaji wao unalenga pia kushirikisha wakulima wadogowadogo.

No comments:

Post a Comment