Tuesday, March 18, 2014

WASINDIKAJI MPUNGA WAANZISHA UMOJA




WASINDIKAJI wa zao la mpunga Jijini Mbeya wameanzisha umoja wao ili uweze kuwasaidia kupata soko la uhakika la ndani na nje ya nchi pamoja na kuwa na nguvu ya pamoja ya kutatua matatizo ya wasindikaji wa zao hilo. 

Imeelezwa kuwa wasindikaji wa mpunga wamekuwa katika mazingira magumu ambapo mchele unakuwa hauna ubora kutokana na kila mkulima kuzalisha anavyojua hivyo kuwa na chombo cha pamoja kutaweza kusaidia kuwa usindikaji bora wa zao hilo. 


Hayo yamesemwa juzi na Mwenyekiti wa muda wa Umoja wa wasindikaji wa Mpunga Jijini humo, Peter Mlegula wakati wa mkutano wa wasindikaji hao uliofanyika jijini Mbeya. 


Mlegula alisema kuwa bado kuna changamoto nyingi kwa upande wa wasindikaji lakini kwa nguvu ya pamoja itaweza kusaidia kufika pale wanapohitaji ili kuweza kutatua kero za wasindikaji wa mpunga ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikiwakabili . 


"Huu umoja tulioanzisha utakuwa na manufaa makubwa sana kwetu sisi wasindikaji kwani hivi sasa tumepata chombo cha pamoja cha kusemea kero zetu ambapo hapo awali hatukuwa na sehemu yeyote ya kusemea," alisema Mwenyekiti huyo. 


Msindikaji mwingine Diana Mwaisabila kutoka Wilaya ya Mbarali alisema kuwa lengo la kuanzisha umoja huo ni baada ya kuona wasindikaji wa zao la mpunga hawana mwelekeo wowote kwani kila mmoja anasindika zao hilo anavyojua. 


Alisema kuwa umoja huo utaweza kuwasaidia kukaa pamoja na shirika la umeme Tanesco kujadili ongozeko la umeme ambalo kwa kiasi kikubwa limekuwa likiwanyonya wasindikaji wa zao la mpunga.
Kwa upande wa msindikaji mwingine, Abel Mwakipesile alisema kuwa kama msindikaji amefarijika sana kuwa na chombo chao ambacho kitaweza kusaidia hata serikali kuwatambua ili waweze kusaidiwa. 


Mkutano huo wa siku moja wa wasindikaji wa zao la mpunga mkoani Mbeya uliandaliwa na Shirika la Maendeleo la Uholanzi (SNV) lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wasindikaji kwa kuwa na chombo chao wenyewe.

No comments:

Post a Comment