Thursday, April 25, 2013

Serikali yalaumiwa kupeleka mbolea ‘mbovu’ Nkasi

Mbunge wa Nkasi, Ali Keisy (CCM) ameilaumu Serikali kwa kutokuwa na mpango mzuri kwa wakulima wa Mkoa wa Rukwa, kwani imeshindwa kuwaondolea kero kubwa ya mbolea ya Minjingu ambayo ilipelekwa muda mrefu na kuonekana mbovu.
Keisy alisema Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika ilipanga kuwasaidia wakulima wa ukanda huo mbolea ya ruzuku, lakini ilibainika mbolea yote tani 1,000 iliyopelekwa Mkoa wa Rukwa ilikuwa haifai.
“Hata hivyo, naishangaa Serikali yangu, hivi kweli huyo Minjingu ni nani na kwa nini ameiweka Serikali mfukoni kiasi hicho, mbona hamumshughulikii,” alihoji.
Alishangazwa na kitendo cha wizara hiyo kuendelea kuweka mbolea hiyo kwenye maghala kwa muda mrefu, huku wakisingizia kuwa watapeleka mbolea nyingi kuihuisha na kwamba, ni makosa kwani wangepaswa kukamatwa wakati huo baada ya kuifikisha.
Pia, Keisy alilaumu Serikali kwa kuendelea kuagiza mchele kutoka nje ya nchi, ilihali Tanzania kuna mchele mwingi wenye ubora ambao hauna soko.
Keisy alisema kama Serikali itakuwa makini kuwatengenezea miundombinu wakulima wa mpunga, haitapata tabu ya kuagiza mchele kutoka nje ya nchi.
Aliitaka Serikali iwe makini katika suala la kilimo nchini.

No comments:

Post a Comment