Tuesday, February 18, 2014

WIZARA KUNUNUA MAZAO YA NAFAKA NCHINI






Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika imetangaza nia yake ya kutaka kununua mazao ya nafaka ili kumwekea mkulima wa hali ya chini soko la uhakika.
Miongoni mwa mazao yatakayonunuliwa kupitia Bodi  ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko  ni mpunga,maharagwe,karanga,choroko,ulezi,ufuta na mahindi,na yatanunuliwa kwa bei ya ushindani ya soko mwaka huu.
Hayo ni kwa mujibu wa Mchumi wa bodi hiyo Bw. Edwin Mkwenda  katika maonesho ya wakulima yaliyofanyika kitaifa katika Viwanja vya Nzuguni Manispaa ya  Dodoma.
Bw. Mkwenda alisema tayari Serikali imeikabidhi bodi hiyo maghala yote yaliyokuwa ya Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC),ambayo hayakubinafsishwa zilizoko  kwenye kanda saba  ili kutunza mazao yatakayonunuliwa.
Kuundwa kwa bodi hiyo ni ukombozi kwa wakulima kwani watakuwa na uhakika wa kupata soko la mazao husika.



UMWAGILIAJI WA MATONE KUONGEZA UZALISHAJI



Serikali imepanga kuendeleza teknolojia ya Umwagiliaji wa Matone ili kuongeza kiwango cha uzalishaji wa mazao kwa wakulima.
Akizungumza katika kilele cha maonesho ya sikukuu ya wakulima ya Nane Nane katika Viwanja vya Nzuguni mkoani Dodoma, Makamu wa Rais wa pili wa Zanzibar, Balozi Seif Ally Iddy alisema kuwa umwagiliaji kwa njia ya matone utasaidia katika kukuza  uzalishaji wa mazao ya nafaka na bustani.
“Kutokana na teknolojia hii mpya ya umwagiliaji wa matone serikali imeweza kuvuna tani 16,510 za mazao kwa mwaka’’, alisema Balozi Seif.
Aliendelea kueleza kuwa teknolojia ya umwagiliaji ni lazima ipewe kipaumbele na kutekelezwa nchi nzima ili wakulima waweze kuzalisha mazao kwa wingi na kuuza ndani na nje ya nchi.
Aidha Balozi Seif aliwataka waandaaji na waendeshaji wa maonesho ya Nane Nane (TASO)  waweke utaratibu mzuri wa maonesho hayo ili wakulima waweze kuhamasika na kuhudhuria kwa wingi ili wapate mafunzo ya kilimo na ufugaji

No comments:

Post a Comment