Friday, February 20, 2015

Soya zao lenye manufaa lukuki kwa jamii

Soya zao lenye manufaa lukuki kwa jamii



Maharagwe ya soya ni moja ya mazao muhimu katika jamii ya mikunde katika nyanja za uzalishaji wa kibiashara kutokana na kuwa na kiasi kikubwa cha protini (35-40%). Soya inatumika katika kuandaa vyakula vinavyoliwa vikiwa vibichi, vinavyovundikwa na vyakula nikavu, mfano maziwa, tofu, mchuzi pamoja na kimea.


Hali ya hewa, udongo na maji


Soya hulimwa katika ukanda wa Ikweta. Soya hukomaa katika kipindi cha siku 180 (miezi 6) lakini inaweza kuwa na baadhi zinazokomaa mapema zaidi. Joto chini ya nyuzi joto 21 na juu ya 32 inaweza kuathiri ushavushaji na utengenezaji wa viriba. Na joto zaidi ya nyuzi 40 ni hasara kwa uzalishaji wa mbegu.


Endapo maji yanapatikana, Soya inaweza kulimwa kwa kipindi chote cha mwaka. Soya huhitaji milimita 400-500 za maji kwa msimu ili kupata mazao bora. Kiwango cha juu cha unyevu kinahitajika sana wakati wa kuota, kuchanua na kuunda viriba. Hata hivyo majira ya kiangazi ni muhimu kwa ajili ya kukomaza. Soya inaweza kuvumilia maji yaliyotuama lakini mvua ikizidi ni tatizo kubwa kwa uzalishaji wa mbegu.






Kupanda


Soya inapandwa kwa kutumia mbegu. Hata hivyo mbegu za soya hupoteza uwezo wake katika kipindi cha miezi 6-10, kulingana na aina, hali ya hewa mazingira, na joto hasa kwa sehemu ambayo hazikuhifadhiwa vizuri. Pima uwezo wa mbegu kabla ya kupanda:


Chukua punje 100 kutoka maeneo 3 tofauti ya mbegu, weka punje hizo 100 kutoka kila kundi kwenye glasi ya maji kwa saa 24, toa maji yote kisha weka pamba au kipande cha nguo chakavu.


Baada ya siku 3 mbegu zitaanza kuchipua na ni rahisi kuweza kuhesabu ni mbegu ngapi zimeota kutoka katika kila kundi. Mbegu zilizoota kwa zaidi ya 85% zinahesabika kuwa mbegu bora. Unaweza kupanda katika majaruba. Soya hupandwa katika nafasi ya sentimita 25×25 au 20×20. Katika ardhi iliyotifuliwa unaweza kusia mbegu za soya katoka umbali wa sentimita 40-50. Unaweza pia kupanda katikati ya mistari ya mazao mengine umbali wa sentimita 10. Nchini Tanzania inashauriwa kupanda Soya aina ya Uyole.


Kulima kwa Mseto


Soya inalimwa kama zao linalojitegemea au kama zao mseto. Kwenye mahindi na mtama, soya inaweza kupandwa mistari miwili. Kupanda soya mseto na mahindi huvutia nyigu ambao husaidia kudhibiti minyoo ya mahindi (African boll worm) na wakati huo huo husaidia kuzuia magugu kuota. Soya isipandwe sehemu moja mfululizo kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili ili kuzuia magonjwa kwenye udongo. Panda mazao kwa mzunguko katika kipindi cha miaka 3 mpaka 4 ili kuzuia magonjwa. Mzunguko usifuatiwe na maharagwe ya kula au alizeti kwani yanaweza kuchukua ugonjwa wa ukungu mweupe.


Matunzo


Kuandaa kitalu mapema na kuondoa magugu yote ni mwanzo wa mavuno mazuri. Kunyeshea wakati wa kuchanua na wakati wa kupanda ni muhimu ili kupata kiwango cha juu cha mavuno. Umwagiliaji unahitajika kwenye udongo wa kichanga na aina nyingine ya udongo unaopitisha maji kirahisi kuliko kwenye udongo wa mfinyanzi. Soya ina uwezo mkubwa wa kupata nitrojeni kutoka hewani, ambapo husaidia kuua bakteria walioko kwenye udongo.


Mahali ambapo soya haijawahi kupandwa ni vyema ukapanda Soya maalumu yenye kinga (unaweza kuwasiliana na wataalamu wa kilimo walio karibu kwa ushauri zaidi). Hata hivyo, ni muhimu kuongeza mbolea ya fosiforasi ili kusaidia kutengeneza mizizi pamoja na ukuaji wake.


Mavuno


Ukipanda aina inayokomaa haraka unaweza kupata mavuno katika kipindi cha siku 70, na aina inayochelewa kukomaa unaweza kupata mavuno katika kipindi cha siku 180. Unaweza kuvuna kwa kukata mmea kwenye shina ama kung’oa pamoja na mizizi yake wakati ambao majani yameanza kukauka na kuwa na rangi ya kahawia, na pia walau kiriba kimoja kiwe kimekauka kutoka katika kila


shina. Soya inayoliwa kama mbogamboga, huvunwa wakati bado ikiwa mbichi lakini viriba vikiwa tayari vimejaa punje. Wakulima wadogo wadogo walio wengi huweza kuvuna kiasi cha kilo 400-500 kwa ekari, ingawa inawezekana kupata kilo 3000 endapo utafuata vizuri taratibu za kupanda, mbegu nzuri, palizi na matunzo kwa ujumla.


Uhifadhi


• Acha maharage yakauke kiasi cha kuwa na unyevu chini ya asilimia 12 kabla ya kuyahifadhi.
• Weka kwenye stoo safi na kavu ili kuzuia wadudu kuingia.
• Punje zinazokusudiwa kutumika kama mbegu zisihifadhiwe kwa zaidi ya mwaka mmoja.




No comments:

Post a Comment