Tuesday, May 7, 2013

Grace Kihwelu alilia zao la kahawa

Dodoma
Mbunge wa Viti Maalum, Grace Kihwelu (Chadema) ameitaka Serikali kuja na mpango madhubuti wa kufufua kilimo cha kahawa katika Mkoa wa Kilimanjaro.
Akiuliza swali bungeni jana,mbunge huyo alisema kwa miaka mingi zao hilo limekuwa tegemeo kwa wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro,lakini kwa sasa kilimo hicho ni kama kimekufa.
“Je Serikali ina mpango gani madhubuti na mahsusi wa kufufua kilimo cha kahawa Kilimanjaro ambacho kwa miaka mingi kimekuwa tegemeo kwa wananchi wa Kilimanjaro na mhimili mkubwa kwa uchumi wa taifa?” Alihoji Kiwelu.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira alisema Serikali imeandaa mkakati wa kuendeleza tasnia ya kahawa kwa lengo la kuendeleza kilimo cha kahawa nchini kwa kuongeza tija na ubora wa kahawa kitaifa.
Aliyataja maeneo mahsusi ya mkakati huo ni pamoja na kuongeza uzalishaji wa kahawa safi kutoka wastani wa sasa wa tani 50,000 kwa mwaka hadi tani 100,000 ifikapo mwaka 2022.
Nyingine ni kuongeza ubora wa kahawa ili kupata bei ya ziada katika masoko ya nje kutoka wastani wa asilimia 35 hadi kufikia wastani wa asilimia 70 ifikapo mwaka 2022,” alisema
Alisema maeneo muhimu katika mkakati huo ni pamoja na kuimarisha huduma za ugani ili wakulima wazingatie kanuni bora za kilimo cha kahawa na kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (TaCRI) ili kuhakikisha upatikanaji wa miche bora ya kahawa.
Wassira alisema pia serikali inaendelea kuongeza matumizi ya viwanda vya kati vya kutayarisha kahawa ili kuongeza ubora wa zao hilo hivyo wakulima kunufaika na bei nzuri.

No comments:

Post a Comment