Saturday, May 11, 2013

Waziri Chiza kuzindua bodi mpya ya kahawa

 
Bodi mpya ya Wakurugenzi wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), itazinduliwa wiki ijayo mjini Dodoma na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Astery Bitegeko, alithibitisha jana kuwa uzinduzi wa bodi hiyo ambao umepokewa kwa furaha na wakulima wa kahawa nchini utafanyika Jumatano ijayo.
Kuvunjwa kwa bodi ya awali kulitokana na malalamiko kutoka kwa wakulima akiwamo Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi aliyedai uteuzi wake ulikiuka sheria ya kahawa ya mwaka 2001.
Wajumbe wapya wa bodi hiyo ni Dk Juma Ngasongwa anayekuwa mwenyekiti na Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Adolf Kumburu anayekuwa katibu wa bodi hiyo.
Wengine na taasisi wanazotoka zikiwa kwenye mabano ni Novatus Tiigelerwa (Kdcu), Profesa Suleiman Chambo (Muccobs), Thahir Nzalawahe na Philip Mbogela kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika.
Profesa Chambo na Mbogela wameingia katika bodi hiyo kama wataalamu wa zao la kahawa linalokabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwamo kuongeza uzalishaji, ubora na kusaka masoko mapya.
Wajumbe wengine ni Fatima Faraji (TCGA), Hyasinth Ndunguru (Kimuli Amcobs), Amir Hamza (TCA) na Maynard Swai kutoka Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro (KNCU).

No comments:

Post a Comment