Saturday, May 11, 2013

Wakulima 3,000 kunufaika na kilimo shadidi

WAKULIMA 3,000 wa zao la mpunga katika vijiji vinane vilivyopo Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, watanufaika na mfumo wa kilimo shadidi (System of Rice Intensification (SRI) kuanzia msimu ujao wa kilimo.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Iringa, Elvin Mwakajinga, alibainisha hayo kwenye maadhimisho ya Siku ya Mkulima yaliyofanyika katika Kijiji cha Makifu na kuwakutanisha baadhi ya wakulima wa mpunga wa Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, Mbarali, mkoani Mbeya na Iringa.
“Kunufaika kwa wakulima hao ni matokeo ya mafunzo ya kuanzishwa kwa mfumo huo katika Wilaya ya Iringa yaliyoendeshwa kwa wakulima 512 na Taasisi ya Maendeleo Mijini na Vijijini (RUDI) Novemba, mwaka jana na kufuatiwa na mashamba darasa 50 msimu huu wa kilimo,” alisema Mwakajinga.
Mwakajinga alisema ni jambo jema kwa mfumo huo kuwafikia wakulima wengi na ikiwezekana wote na kuwataka watendaji wa vijiji na kata kuanzisha na kufufua vikundi vya wakulima, ili wawe na nguvu ya pamoja.
Mtendaji Mkuu wa RUDI, Abel Lyimo, alisema katika maeneo ambayo mfumo tayari unatumika kama Kilombero na Mbarali, uzalishaji umefikia magunia 40 kwa ekari moja.
Kwa upande wao, wakulima hao walisema mfumo utawasaidia kuongeza kipato cha kaya na taifa kwa jumla na kuiomba serikali kusaidiana na taasisi ya RUDI kueneza mfumo huo kwa wakulima wote nchini.

No comments:

Post a Comment