WAKULIMA nchini wametakiwa kuzingatia ushauri wa watafiti na wataalam
mbalimbali wa kilimo waweze kuzalisha mazao bora yenye tija katika soko
la Afrika Mashariki (EAC).
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kimataifa
ya Utafiti wa Kilimo (IITA), Dk.Victor Manyong alisema endapo wakulima
watazingatia ushauri watazalisha bidhaa bora zenye kukidhi matakwa ya
walaji na hatimaye kuzalisha faida itakayowakwamua wao na familia zao.
Alisema
IITA imekuwa ikifanya utafiti katika nchi mbalimbali za EAC kwa
wakulima wadogo na kwa Tanzania tangu utafiti wa kilimo uanze mwaka 1994
kwa zao la mihogo na imeweza kuwaelekeza wakulima ni mbegu zipi zinafaa
kulingana na ardhi yao.
“Kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo
tumejikita katika utafiti mbalimbali na lengo kuu ni kuwasaidia wakulima
waweze kulima kilimo cha kisasa kwa kutumia mbegu bora ambazo
zitawasaidia kujiongezea kipato na kuachana na tabia ya kulima kwa
mazoea,”alisema Manyong.
Alisema si kila mbegu au ardhi inafaa
kwa kila zao hivyo kila fursa iliyopo inatumiwa kufanya utafiti na
kugawa aina ya mazao yanayoonekana ni bora kwa majaribio kwa kuwapa
wakulima ili na wao wajaribu na kutoa maoni yao.
Manyong alisema
katika mkakati huo hadi sasa taasisi imeweza kubaini mbegu 18 za mihogo
ambazo ni bora na zifaa kwa mkulima kupanda na kuzalisha faida kwa wingi
endapo atazingatia maelekezo ya wataalam.
Alisema ili kuendelea
kutoa huduma bora kwa wakulima nchini taasisi imejenga jengo lenye
maabara ya kisasa la utafiti ambalo linatarajiwa kulizinduliwa Mei 13
mwaka huu na Rais Jakaya Kikwete.
Manyong alisema kuzinduliwa kwa
jengo hilo kutasaidia kuwapa uelewa zaidi wanafunzi na watalaam wa
utafiti mbalimbali wa kilimo nchini.
No comments:
Post a Comment