Friday, February 27, 2015

Wakulima wadogo wabadili mwelekeo wao wa kilimo

SIMU za mkononi ni muhimu zaidi hivi sasa kwa wakulima katika wilaya za Mbeya, Mbarali na Morogoro baada ya kuanza kuzitumia kupata taarifa mbalimbali za masuala ya kilimo.
Matumizi hayo ya wakulima kwa baadhi ya vijiji katika wilaya hizo yanabainisha kuwapo kwa mahitaji ya vipindi vya kilimo katika vyombo vya habari nchini, kutokana na uwepo wa wafuatiliaji wa karibu kwa vipindi hivyo.
Katika baadhi ya vijiji ndani ya wilaya hizo tatu, wakulima hufuatilia vipindi vya kilimo vinavyotolewa katika redio maalumu walizochagua na hutumia simu za mkononi kuwasiliana na waendeshaji vipindi hivyo au wataalamu wao wa kilimo kwa ajili ya kupata taarifa za kilimo anazozihitaji.
Farm radio ni vipindi vinavyorushwa redioni kupitia mradi maalumu wa kuwajengea uwezo wagani katika kuendeleza matumizi ya mikunde kurutubisha udongo nchini, unaotekelezwa kwa ufadhili wa Shirika la Mapinduzi ya Kijani Afrika (AGRA).
Kupitia mradi huo, baada ya wagani hao kupatiwa taaluma ya kurutubisha udongo huisambaza kwa wakulima katika maeneo yao kupitia vipindi vya redio na simu za mkononi na kisha, wakulima nao hupata nafasi  kuwasiliana na wataalamu hao kuhusu masuala mbalimbali ya kilimo kupitia vyombo hivyo.
Kwa mujibu wa Ofisa Mradi huo, Christopher Mkondya, wakulima 260 kutoka vijiji vya Nsongwi, Ifiga na Nsongwi Juu, katika Wilaya ya Mbeya Vijijini wameunganishwa na redio ya Baraka FM kupitia vikundi vyao vya wasikilizaji, na kwa Wilaya ya Mbarali wakulima 160 wameunganishwa na redio Bomba FM.
Wilayani Mbarali, mradi huo unafanya kazi na wakulima waliojiunga katika vikundi vya skimu za umwangiliaji kwa ajili ya kilimo cha mpunga, ambazo ni pamoja na Majengo, Maendeleo na Ruanda Manjenje, ambazo zinahudumia vikundi vya Majengo, Hamasa, Maendeleo na Ruanda Manjenje.
Mbali ya Mbeya, mradi huo pia unahudumia wakulima 160 katika Wilaya ya Kilosa wanaounganishwa na redio ya Aboud FM. Wakulima hao ni kutoka kwenye vijiji vya  Kondoa, Chanzuru na Ludewa.
Hata hivyo, wakulima walioko kwenye masafa ya redio hizo nao wamekuwa wakifuatilia, na hivi sasa mahitaji yanaongezeka kwa kasi ambapo wakulima wengi zaidi kutoka vijiji visivyofikiwa na huduma hiyo, wanashinikiza kuingizwa kwenye mradi ili nao wanufaike na elimu ya kilimo bora inayotolewa kupitia vifaa hivyo vya elekroniki.
“Mwitikio wa wakulima ni nzuri, wanashirikishwa katika vipindi, hujisajili kwenye orodha ya simu ili kupata taarifa mpya za vipindi na taarifa za kilimo,” anasema Mkurugenzi wa Baraka FM, Henry Mazunda.
Watayarishaji wa vipindi hivyo wanathibitisha kuwepo kwa mahitaji makubwa ya taarifa za kilimo, ambapo wakulima wenye kubahatika kunasa mawimbi ya vipindi hivyo huwapigia simu kuomba kushirikishwa kwenye mpango huo pamoja na kupatiwa elimu ya mazao mengine zaidi ya mahindi na yale ya jamii ya mikunde.
“Wakulima wengi zaidi kutoka nje ya mradi wanafuatilia na kuuliza maswali, nao wanataka kushirikishwa kwenye mradi,” anasema Lina Mwambungu, mmoja wa watayarishaji wa vipindi hivyo vya wakulima.
Lina anazitaja taarifa zinazopatikana kupitia ujumbe mfupi wa simu kuwa ni pamoja kukumbushwa siku na muda wa kipindi, elimu kuhusu kilimo bora cha mahindi na mazao jamii ya mikunde, wakulima hutuma maswali kuhusu taarifa wanazohitaji au maombi ya kurudiwa kwa kipindi.
Ofisa ugani kutoka Kijiji cha Mantanji, Wilaya ya Mbeya Vijijini, Abubakar Ramadhan anauona mradi huo kuwa wenye tija kwa wakulima na kubainisha kuwa kwa mkulima mwenye kushiriki kikamilifu kwenye mradi huo huongeza wingi na ubora wa mazao yake.
Anasema shamba lenye mchanganyiko wa mahindi na mikunde huongeza tija katika uzalishaji kutokana na virutubisho vinavyotengezwa na mazao jamii ya mikunde na wakati huo huo hutunza udongo, hauchakai na kupoteza uwezo wake wa kuzalisha.
Katika msimu wa kilimo wa 2012/2013, mkulima kutoka Kikundi Faida Mwandaji, Jela Mandewela alikuwa na ekari moja ya kilimo mseto ambapo alipanda mahindi na maharage, na katika mavuno yake amevuna maharage kilo 300, mahindi ikiwa ni kati ya gunia 22 hadi 26.
Hali hiyo anasema ni tofauti na huko nyuma alipovuna gunia kati ya tatu na saba katika ekari ile ile moja, na wakati huo huo akikosa maharage ambayo alilazimika kuyalima kwenye eneo jingine hivyo kutokuwa na matumizi mazuri ya ardhi.
“Tunapata elimu kutoka kwa ofisa ugavi na vipindi vya redio, tunarekodi mambo yetu ya kilimo, tunatumia simu kuwasiliana na wataalamu wetu na watangazaji,” anasema Mandewele kisha anaongeza akisema; “redio inatusaidi kupata elimu, tunatambulika na watu, wanatusikiliza.”
Rozina Mohamed kutoka Kijiji hicho cha Mantanji anakielezea kilimo mseto kuwa na faida zaidi kwao ambapo anasema tangu aingie kwenye kilimo hicho ameweza kuongeza kipato cha familia yake na sasa anamudu kusomesha watoto wake walioko shule za sekondari.
Manufaa mengine aliyopata ni pamoja na kuezeka bati kwenye nyumba yake, kuweka maji ya bomba na amenunua mifugo ikiwemo ng’ombe na mbuzi, akisisitiza kwamba kilimo kina faida kuliko uchuuzi.
Hata hivyo mradi huo unakabiliwa na changamoto kubwa ya mahitaji kuzidi uwezo uliopo sasa. Mradi unaelekeza darasa moja la maofisa ugani kuwa na watu 40 kwa chuo, lakini kutokana na ongezeko kubwa la mahitaji wamejikuta wakifika hadi 70 lakini wakihudumiwa na rasilimali zile zile za watu 40.
Vyuo vinavyohusika na utoaji elimu hiyo kwa wagani ni MATI Uyole na Igurusi vilivyopo mkoani Mbeya na kile cha Ilonga mkoani Morogoro.
Katika mfumo wa uendeshaji mradi huo, kila chuo kimekuwa kikihudumia vijiji vitatu vinavyokizunguka na kwamba ni wakulima wenyewe ambao huchagua redio ambazo wangependa zitumike kuwarushia matangazo hayo.
Mkondya anasema, uandaaji wa vipindi hivyo hufanywa kwa kushirikiana kati ya wakulima, wagani na watangazaji ambao huwatembelea wakulima kwenye vijiji vyao na kuandaa nao vipindi. 
- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/wakulima-wadogo-wabadili-mwelekeo-wao-wa-kilimo#sthash.O55W8xaH.dpuf

No comments:

Post a Comment