Tuesday, March 4, 2014

AFRIKA YAZINGATIA UCHUMI UNAOJALI MAZINGIRA: UNEP

Profesa Wangari Maathai alikuwa mstari wa mbele kupigania uhifadhi wa mazingira


Shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP limesema bara la Afrika liko kwenye mwelekeo sahihi wa kuchochea shughuli za kiuchumi zinazojali mazingira.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP Achim Steiner amesema hayo leo siku ambayo bara hilo linaadhimisha siku ya mazingira ikiwa ni utambuzi wa mwanaharakati wa mazingira duniani na mshindi wa tuzo ya amani hayati Profesa Wangari Maathai.

Bwana Steiner ametolea mfano matumizi ya nishati ya jua huko Algeria na Tunisia na uwekezaji wa fedha kwenye shughuli za kiuchumi zinajazojali mazingira huko Afrika kusini.

Amesema Profesa Maathai alionyesha aina ya uongozi wenye maono ambao unatakiwa kushinda uharibifu wa mazingira na ni matumaini yake kuwa katika kutambua siku hiyo viongozi wengine wataiga mfano wake ili kulinda maliasili na hivyo kuweka msingi wa mustakhbali endelevu na uhakika wa upatikanaji chakula.

Benki ya dunia imesema Afrika inapitia ukuaji thabiti wa kiuchumi lakini changamoto kama vile mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa mazingira na ujangili wa wanyamapori ni lazima vishughulikiwe ili kuendeleza kiwango cha ukuaji uchumi.

 

No comments:

Post a Comment