Tuesday, March 4, 2014

TIC YAPONGEZA KILIMO CHA MIWA ECOENERGY



KITUO cha Uwekezaji nchini (TIC) kimesifu Kampuni ya EcoEnergy Tanzania kuwa shughuli zake za Kilimo zinazolenga kupunguza tatizo la uhaba wa sukari na nishati ya umeme.
Mkurugenzi wa Mtendaji wa kituo hicho, Juliet Kairuki, alisema hayo wakati alipofanya ziara ya kutembelea shamba kubwa la miwa linalomilikiwa na kampuni hiyo katika Bonde la Mto Ruvu.

"Tumekuja kujionea maendeleo ya shamba hili ambalo ni moja ya miradi mikubwa ya kilimo hapa nchini," alisema, Kairuki. Shamba hilo linazalisha zao la miwa kwa nia ya kuzalisha sukari na kutengezea nishati ya umeme.

Katika ziara hiyo aliambatana na ujumbe wa wafanyabiashara kutoka mji wa Vallejo ulipo jimbo la California Marekani ambao walikuwa wakiongozwa na Meya wao, Osby Davis.
Alisema wafanyabiashara hao walitembezwa katika mradi wa shamba hilo la miwa kwa nia ya kuwavutia kuja kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali ikiwemo ya Kilimo.

"Mradi huu unatarajia kuajiri watu wengi," alisema. Kairuki aliwaambia wafanyabiashara hao kuwa serikali inatoa vivutio mbalimbali vya uwekezaji, na kufanikiwa kwa mradi wa shamba hilo la miwa ni matokeo ya vivutio hivyo.

Alisema mradi huo una manufaa makubwa kwa taifa kwa kuwa utasaidia kuleta ujuzi na teknolojia kuhusiana na kilimo cha kisasa cha miwa hapa nchini.
Naye Meya Davis alisifu harakati zinazofanywa na Tanzania katika kuinua Kilimo na shughuli nyingine za biashara na uchumi zinazofanyika hapa nchini.

"Tumejionea mradi huu mradi huu wa miwa unavyoendelea... ni matumaini yangu umewavutia wafanyabiashara toka Vallejo kuja kuwekeza Bagamoyo," alisema.
Katika hatua nyingine Meya huyo pia alitumia ziara hiyo kutembelea shule za Msingi Majengo na Mbaruku za mji wa Bagamoyo na kutoa zawadi mbalimbali.

"Tunatambua kuwa njia kuu ya kupata maendeleo na kukuza uchumi ni kuwekeza katika elimu," alisema na kuongeza kuwa wameamua kusaidia kuwekeza katika watoto hao.
Alisema misaada hiyo waliyoitoa ni sehemu ndogo tu, kwa kuwa mji wa Bagamoyo na Vallejo ni marafiki, hivyo uongozi wa mji huo unalenga kuleta maendelea zaidi ya kiuchumi na kijamii katika mji wa Bagamoyo.

Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) kiliandaa ziara ya ujumbe wa wafanyabiashara kutoka mji wa Vallejo ambao walitembelea miradi mbalimbali ya maendeleo katika mji wa Bagamoyo.

No comments:

Post a Comment