Friday, March 7, 2014

WANAVIJIJI WENGI ZAIDI WA CHINA WAANZA KUFANYA BIASHARA KUPITIA INTERNET




Bibi Li Haibo ni ofisa wa kamati ya kijiji kimoja kilichoko kaskazini mashariki mwa China. Mwezi huu amepata kazi mpya, ambayo ni kuwafundisha na kuwaelekeza wanakijiji kufanya biashara kupitia Internet, ili kuwasaidia kuongeza kipato chao.

Mwishoni mwa mwezi Februari, mkoa wa Jilin ulifanya mkutano wa mafunzo ya wafanyabiashara kupitia Internet. Viongozi wa idara za biashara za kaunti mbalimbali na wahitimu wa vyuo vikuu wanaofanya kazi katika kamati za vijiji mkoani humo, walikusanyika pamoja kusikiliza mafunzo ya wataalamu wa kampuni ya Alibaba ambayo ni kampuni maarufu inayotoa huduma ya biashara kupitia Internet nchini China.

Mkoa wa Jinlin ambao unazalisha mazao ya kilimo kwa wingi lakini uchumi hake haujaendelezwa vizuri, ulipanga kuwasaidia wakulima katika vijiji 100 kufanya biashara ya bidhaa zenye sifa ya kipekee za huko kupitia Internet.

Takwimu zilizotolewa na kituo cha utafiti cha Ali kinachomilikiwa na kampuni ya Alibaba zinaonesha kuwa, hadi tarehe 30 Novemba mwaka 2013, maduka ya ngazi ya vijiji na miji midogo yaliyosajiliwa kwenye tovuti ya Taobao.com yalikuwa milioni 1.05. Idadi hiyo iliongezeka kwa laki 4 na 60 elfu kuliko mwaka 2012, ambalo ni ongezeko la asilimia 76.3.



Bibi Li Haibo sasa ni naibu katibu wa kamati ya chama ya kijiji cha Erdaohezi mjini Dunhua mkoani Jilin. Ni mhitimu wa chuo kimoja cha uchumi, na alianza kufikiria njia ya kuwasaidia wanakijiji kuuza mazao ya ginseng na uyoga mweusi.

Bibi Li anasema, hata katika vijiji viliyoko nyuma kiuchumi, watu wananunua bidhaa kwa wingi kupitia Internet, na makampuni mbalimbali ya usambazaji wa vitu yameanzisha matawi yao vijijini, hivyo biashara kupitia Internet ina mustakabali mzuri.

Gongzhuling ni moja ya kaunti zilizoko mkoani Jilin. Mamia ya makampuni ya huko yameanza kuuza bidhaa zao kupitia Internet, lakini bidhaa nyingi zinauzwa katika kaunti hii tu.
Mkurugenzi wa idara ya biashara Bw. Sun Dianpu ana mpango wa kuwaelekeza wazalishaji na wauzaji kujifunza ujuzi kuhusu biashara kupitia Internet, kuanzisha maduka kwenye tovuti, na kuuza mahindi na maharagwe yanayozalishwa huko nchini kote.

Katika mikoa ya pwani ya Jiangsu, Zhejiang na Shandong, baadhi ya vijiji vimepewa jina la "vijiji vya Taobao", kwa sababu maelfu ya wanavijiji wameanzisha maduka yao kwenye tovuti ya Taobao.com.

Ripoti ya maendeleo ya biashara kupitia Internet katika kaunti za China mwaka 2013 iliyotolewa na kituo cha utafiti cha Ali mwezi Januari inaonyesha kuwa, kati ya kaunti 100 zinazopata maendeleo zaidi katika biashara kupitia Internet, kauti 49 ni za mkoa wa Zhejiang.

Katika kijiji cha Liucun mjini Yiwu mkoani Zhejiang, karibu kila familia inashughulikia mauzo ya bidhaa kupitia Internet. Thamani ya mauzo ya maduka zaidi ya 2000 ya wanakijiji hao ilikuwa yuan bilioni 2 mwaka jana.

Mkoa wa Jilin pia umechukua hatua ya kujenga "vijiji vya Taobao" na kaunti za biashara kupitia Internet. Jumba la Jilin ni moja kati ya jukwaa kubwa la biashara linalojengwa.

Mkurugenzi wa idara ya biashara ya Jilin Bibi Cong Hongxia anasema, jumba hilo litakusanya bidhaa kutoka sehemu mbalimbali, zikiwemo mchele, maharagwe, ginseng, vyura, maji yenye madini, uyoga mweusi na matunda ya blueberry yanayozalishwa kwenye mlima Changbai.

Naibu meneja mkuu wa kampuni ya Alibaba Bw. Gao Hongbing anasema, mikoa ya pwani iliyoko kusini mashariki mwa China imetangulia kuendeleza biashara kupitia Internet na imepata maendeleo ya kasi. Ingawa mikoa iliyoko kaskazini mashariki na kaskazini magharibi mwa China ilichelewa kuendeleza shughuli hizi, lakini bado inaweza kupata fursa nyingi.

Takwimu za kituo cha utafiti cha Ali zinaonesha kuwa, hadi mwezi Desemba mwaka jana, China imekuwa na "vijiji 20 vya Taobao", ambavyo viko katika mikoa saba ikiwemo Hebei, Shandong, Jiangsu, Zhejiang na Guangdong. Wanavijiji wa vijiji hivyo wameanzisha maduka elfu 15 kwenye tovuti ya Taobao.com ambayo yanashughulikia mauzo ya bidhaa za majumbani, nguo, mifuko, mazao ya kilimo, bidhaa ndogondogo, na vitu vinavyotumiwa wakati wa michezo au utalii. Shughuli hizi zimewasaidia wanakijiji elfu 60 kupata kazi.

Kituo cha utafiti cha Ali kinasema, kama zaidi ya asilimia 10 ya watu katika kijiji kimoja wanafanya biashara kupitia Internet, na thamani ya mauzo inazidi yuan bilioni 10, basi kijiji hicho kinaweza kuitwa "kijiji cha Taobao".

Wataalamu wanaona kuwa, wanavijiji wengi kufanya biashara kupitia internet ni jambo la kipekee nchini China, na mwaka huu biashara hiyo itaendelea kupata maendeleo ya kasi.

No comments:

Post a Comment