Alizeti haitoi
mailisho pekee, pia inatoa mafuta bora kwa afya ya binadamu na pia
malighafi inayotumiwa na nyuki kutengeneza asali.
Unapotengeneza chakula cha mifugo
peke yako, si tu kupunguza gharama, lakini pia inakupa uhakika wa kuwa na
chakula bora. Pia Wafugaji wa nyuki wanaopanda alizeti wanapata faida ya ziada
kwa kupata asali iliyo bora kwa sababu nyuki hukusanya poleni kutoka kwenye
alizeti wanapofanya ushavushaji.
Chanzo kizuri cha protini
Chakula cha mifugo
kinachotengenezwa kutokana na alizeti ni chanzo kizuri cha protini kwa ajili ya
mifugo, hasa ng’ombe wa maziwa, kuku, nguruwe na hata sungura. Malisho haya
yana kiasi kikubwa cha protini, nyuzi nyuzi na kiasi kikubwa cha mafuta.
Malisho haya yana protini kiasi cha asilimia 29-30, kiasi cha nyuzi nyuzi
asilimia 27-31.
Moja ya tabia nzuri ya alizeti ni
kwamba haina vitu vinavyoathiri virutubisho kwa mifugo, hata hivyo, ina kiasi
kikubwa cha nyuzi nyuzi na mashudu yake kuwa magumu kiasi, jambo ambalo
husababisha ugumu kidogo kwenye kusagwa tumboni. Mbali na virutubisho vya aina
nyingine, alizeti ni chanzo kizuri cha kalishamu, fosiforasi na vitamini B.
Ubora wa alizeti inayotumika kwa
ajili ya malisho ya mifugo inategemeana na namna ambayo imetayarishwa. Kwa
mfano, alizeti inayosagwa bila kuondoa maganda ya nje, ina kiasi kikubwa cha
nyuzi nyuzi (kati ya asilimia 27-30, lakini inakuwa na kiasi kidogo cha protini
asilimia 23). Alizeti ambayo imetayarishwa kwa ubora wa hali ya juu huwa
maganda yameondolewa na inakuwa na kiasi kikubwa cha protini, kiasi cha
asilimia 40.
Mkulima anapaswa kufahamu kuwa
alizeti bado inakuwa na virutubisho hata kama haitatayarishwa kwa ustadi.
Mfugaji anaweza kutumia soya na karanga badala ya alizeti, lakini ni lazima
apeleke alizeti kupima kuhakikisha kuwa ina nyuzinyuzi na virutubisho kwa
kiwango cha nyuzinyuzi na protini kinachokubalika.
Inapendekezwa kutumia alizeti
Kulingana na utafiti ambao
umefanyika nchini Tanzania, alizeti iliyochanganywa na pumba ya mahindi kwa
kiasi cha asilimia 30, kisha kulishwa ng’ombe aina ya Zebu ina uwezo wa
kuongeza uzalishaji wa maziwa kutoka lita 6.6 kwa siku mpaka lita 8.1 kwa siku.
Nchini Zimbabwe, mashudu ya alizetu huchanganywa na mahindi pamoja na
mabua ya mahindi ambayo yamewekwa urea kwa kiwango cha wastani wa kilo
4.4 kwa siku, na kulishwa ng’ombe aina ya Jersey pamoja na ng’ombe chotara
ambao hulishwa katika machungo ya wazi, Ng’ombe hawa huongeza kiasi cha maziwa
kwa wastani wa kilo 5.8 mpaka kilo 6 kwa siku.
Aina ya alizeti
Kuna aina mbili za alizeti,
alizeti fupi na alizeti ndefu. Aina ndefu hurefuka mpaka kufikia kiasi cha
urefu wa mita 1.5-2.4. Uzalishaji wake ni hafifu ukilinganisha na mbegu za
kisasa. Aina hii mara nyingi huwa ile inayojulikana kama Hungary nyeupe na
Fedha. Alizeti fupi ni inayotokana na mbegu za kisasa ambayo huwa na urefu wa
mita 1.2, aina hii huwa na mavuno mazuri zaidi ukilinganisha na aina ndefu.
Kutengeneza chakula cha mifugo
Kilo tatu na nusu za alizeti
inapokamuliwa hutoa mafuta lita moja na mashudu kilo mbili na nusu.
Resheni kwa ng’ombe wa maziwa
•Changanya kilo 18 za mashudu ya
alizeti na kilo 100 za pumba ya mahindi ili kutengeneza chakula cha ng’ombe.
•Mlishe ng’ombe anaezalisha
maziwa kwa wingi kiasi cha kilo 4 ya mchanganyiko huo na kilo 2 kwa ng’ombe
anaezalisha kiasi kidogo cha maziwa.
•Mbali na kulisha mchanganyiko
huo, ng’ombe wa maziwa ni lazima apewe kiasi kingine cha chakula cha kawaida
cha kila siku kama vile matete, hay, au aina nyingine yoyote ya malisho bora
kwa kiasi cha kutosha.
Resheni kwa ajili ya kuku
Chakula cha kuanzia: Changanya kilo 22 za mashudu ya alizeti na kilo
100 za pumba ya mahindi Chakula cha kukuzia: Changanya kilo 20 za mashudu ya
alizeti na kilo 100 za pumba ya mahindi au chenga.
Chakula kwa ajili ya kuku
wanaotaga: Changanya
kilo 18 za mashudu ya alizeti na kilo 100 za chenga za mahindi
ZINGATIA: Unapotengeneza chakula kwa ajili ya ng’ombe wa
maziwa, mfugaji ni lazima ahakikishe kuwa mashudu hayazidi asilimia 20 ya
resheni ya kulishia. Kwa ajili ya kulishia kuku, alizeti isizidi asilimia 7 ya
jumla ya resheni.
Namna ya kuzalisha alizeti
Hali ya hewa: Alizeti hustawi
vizuri zaidi kwenye udongo tifutifu, wenye rutuba ya kutosha. Zao hili lina
mizizi inayoenda chini kwa kiwango cha kikubwa hivyo kuiwezesha kustawi hata
katika sehemu yenye kiwango kidogo cha mvua. Kiasi cha wastani wa milimita
500-750 za mvua zinatosha kabisa kwa uzalishaji wa alizeti. Inaweza kulimwa
kutoka usawa wabahari mpaka kufikia mwinuko wa mita 2600 kutoka usawa wa
bahari.
Maandalizi ya shamba
Ni lazima kuhakikisha kuwa shamba
limelimwa vizuri, ili kuweza kupata sehemu nzuri ya kusia mbegu.
Nafasi: Mbegu zinaweza kupandwa kwa nafasi ya sentimita 75
kwa 30 kwa kiasi cha kilo 2 kwa ekari moja (sawa na kilo 5 kwa hekari). Panda
mbegu 3 kwa kila shimo, kisha acha mmea mmoja kwa kila shimo mimea inapofikia
urefu wa sentimita 10-20.
Matumizi ya Mbolea
Alizeti hufanya vizuri kwenye
udongo wenye rutuba. Matumizi ya mbolea inayotokana na miamba aina ya fosifeti
inafaa zaidi kwa kuwa alizeti inahitaji fosifeti kwa kiasi kikubwa. Matumizi ya
mbolea mboji iliyoandaliwa vizuri itaongeza virutubisho vya ziada kwenye
udongo.
Alizeti hukua vizuri katika
sehemu isiyokuwa na magugu. Palilia alizeti inapokuwa na urefu wa mita 0.7
(Kiasi cha wiki 4).
Ndege waharibifu
Ndege wanaweza kuharibu kiasi cha
asilimia 50 ya alizeti endapo hawatafukuzwa. Ili kuzuia uharibifu huo, mkulima
anaweza kuchukua hatua zifuatazo;
•Vunja shina la alizeti kufikia
usawa wa magoti kabla ya alizeti kukauka. Unaweza pia kuvunja katika urefu wowote
lakini alizeti iangalie chini ili kuzui ndege kudonoa.
• Ondoa alizeti shambani baada ya
kukauka na kuihifadhi.
• Ubanguaji unaweza kufanyikia nyumbani kwa kutumia
fimbo
• Alizeti ni lazima ikaushwe mpaka kufikia kiwango
cha unyevu wa asilimia 10 kabla ya kuhifadhiwa
No comments:
Post a Comment