Tuesday, March 4, 2014

PIS YAANDAA KONGAMANO KWA WAJASIRIAMALI


TAASISI ya kukuza ushirikiano wa Kimataifa wa Israel (PIS) kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) imeandaa kongamano la siku nne linalo wahusisha wawekezaji na wajasiriamali wadogo kutoka katika sekta mbalimbali nchini.

Hayo yamesemwa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi (KLNT), Ibrahim Kaduma alisema kuwa fursa hiyo inakusudia kuleta pamoja watunga sera wataalamu wenye viwanda ili kuweza kushiriki kibiashara katika uwekezaji.
Alisema kuwa kongamano hili linakusudia kujifunza na kuchukua fursa ya maendeleo ya Israel katika ubunifu wa kisayansi na kiteknolojia kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi nchini.
"Kwa misingi hii kongamano linatarajiwa kuendeleza ushirikiano wa kimkakati na ushirikiano imara wa kibiashara na uwekezaji kati ya wajasiriamali na wawekezaji wadogo kati ya Tanzania na Israel," alisema Kaduma.
Aliongeza kuwa kongamano hilo litajikita kwenye sekta ya kilimo, elimu, afya, madini, huduma za fedha, maendeleo ya miundombinu, ujenzi, nishati, teknolojia, viwanda, uhandisi kemikali, biashara, utali pamoja na teknolojia ya habari na mawasiliano.
Naye Mkurugenzi wa huduma na taarifa katika Taasisi ya sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Louis Accaro alisema kuwa taasisi hiyo imefanya mazungumzo na serikali kwa lengo la kufanya usawa katika uwekezaji huo.
Alisema kuwa kwa kusaidiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIS) sera yao imefanikiwa katika suala la uwekezaji.
"Kongamano hili limekuja muda mwafaka katika sekta ya uwekezaji na sisi kama TPSF tumeamua kufanya mambo manne ikiwemo kuanda kongamano pamoja na wafanyabiashara wa Israel na Tanzania kushirikiana," alisema Accara.
Kongamano hilo linatarajiwa kufanyika Machi 17 hadi 20, mwaka huu  ambapo litahusisha wataalamu mbalimbali pamoja na wanenaji 48 katika sekta mbalimbali ambapo wawekezaji na wafanyabiashara zaidi ya 50 watakuwepo katika kongamano hilo.

No comments:

Post a Comment