Serikali inapenda kuwaarifu waombaji
wa nafasi za kazi kwa tangazo la tarehe 27 Novemba, 2013 wa kada za Kilimo,
Mifugo, Uvuvi na Udereva kuwa usaili utaanza tarehe 4 Machi, 2014 takriban
katika mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar.
Katibu wa
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi amesema hayo leo
ofisini kwake wakati akiongea na baadhi ya wadau waliomtembelea kwa lengo la
kufahamu masuala mbalimbali ya uendeshaji wa mchakato wa ajira serikalini.
Amesema usaili huo unaoanza tarehe 4
Machi katika mikoa takribani yote nchini utahusisha jumla ya
wasailiwa 6,087 wa fani za Kilimo, Mifugo, Uvuvi na udereva kwa kada
ambazo sio za Maofisa. Amefafanua kuwa vigezo vya kupanga mikoa ya usaili vimetokana
na anwani ambazo waombaji waliwasilisha katika barua zao za maombi husika ya
kazi.
Daudi alibainisha kuwa kila mwombaji aliyekidhi
vigezo na kuchaguliwa kwa ajili ya usaili anapaswa kwenda kufanyia usaili
katika mkoa aliopangiwa kama anwani yake inavyoonyesha katika tangazo kwenye
tovuti ya Sekretarieti ya Ajira, isipokuwa kwa waombaji wa mkoa wa Katavi wao
wataenda kufanyia usaili mkoa wa Rukwa na waombaji waliotumia anwani za mkoa wa
Singida wao watafanyia usaili mkoa wa Manyara kutokana na sababu zisizozuilika.
Aliongeza kuwa kwa mwombaji ambae hatazingatia
anwani, siku na muda aliopangiwa na kuamua kwenda mkoa mwingine tofauti na
utaratibu uliopangwa ajue wazi hatasailiwa kwa kuwa ratiba na idadi ya majopo
ilishapangwa kwa kila mkoa na haitabadilishwa ili kuweza kurahisisha kazi hiyo
kukamilika kwa ufanisi.
Aidha, amewataka waombaji wote wa
tangazo hilo kutembelea tovuti ya Sekretarieti ya Ajira ambayo
ni http://www.ajira.go.tz/ wao wenyewe
ili kuweza kujua kiundani endapo wamechaguliwa kufanya usaili, kufahamu tarehe,
mahali na muda wa kuanza usaili ili kuepuka usumbufu usiokuwa na lazima.
Daudi aliendelea kufafanua kuwa kwa
waombaji waliotumia anuani za mkoa wa Dar es Salaam kwa nafasi ambazo sio za
maofisa usaili utafanyika tarehe 11 Machi, 2014.
Aidha, kwa nafasi za Maofisa
Kilimo, Mifugo na Uvuvi wote usaili wao utafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia
tarehe 10 hadi 14 Machi, 2014.
Katibu amewataka waombaji
wote kuhakikisha pindi wanapoenda kwenye usaili wawe wamejiandaa vya kutosha
ikiwemo kubeba nyaraka muhimu hususani vyeti halisi vya taaluma zao maana
vitahitajika kwa ajili ya uhakiki siku ya usaili. Aidha, amewasihi waombaji wa
matangazo mengine ya nafasi za kazi kuwa na subira wakati uchambuzi ukiendelea
na pindi utakapokamilika wahusika watataarifiwa.
Alimaliza kwa kuwasisitiza wadau wa
Sekretarieti ya Ajira kuwa pindi wanapoona matangazo ya kazi, ikiwemo kuitwa
kwenye usaili au kupangiwa vituo vya kazi katika vyombo mbalimbali vya habari
hususani baadhi ya mitandao ya kijamii wajiridhishe kwanza kwa kuangalia
taarifa hizo katika tovuti ya Sekretarieti ya Ajira, ili kuepuka taarifa
zisizokuwa za kweli ambazo zimekuwa zikitolewa nyakati nyingine na baadhi ya
watu wasio waaminifu kwa lengo la kupotosha Umma.
Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.
Ofisi ya
Rais-Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma. 21 Machi, 2014
Kwa maelezo
zaidi; wasiliana na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.
No comments:
Post a Comment