Thursday, March 6, 2014

FRIJI INAYOTUNZA UMEME SAA 10 YAINGIA SOKONI



KAMPUNI ya LG, imezindua friji mpya ambayo ina uwezo wa kuendelea kufanyakazi kwa masaa 10 baada ya umeme kukatika.

Akizungumza Dar es Salaam jana, meneja wa bidhaa za LG Tanzania Mayur Parikh, alisema kuwa friji hiyo ina uwezo mkubwa wa kufanya kazi baada ya umeme kukatika ambapo ina uwezo wa kugandisha kwa muda wa masaa 10 bila umeme.

Alisema kuwa wameamua kuizindua bidhaa hiyo mahususi kutokana na matatizo ya kukatika kwa umeme mara kwa mara ambayo hutokea katika maeneo mbalimbali nchini.

Alisema kuwa tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara, limepelekea kampuni yao kutanua wigo wa matumizi ya bidhaa zao na kuamua kuzindua friji hiyo.

Alisema kuwa teknolojia waliyoitumia katika utengenezaji wa bidhaa hiyo ni ya aina yake ambapo baada ya umeme kukatika friji itaendelea kufanya kazi kwa kutumia mfumo maalumu uliotengenezwa kitaalam.

Alisema kuwa pia friji hiyo inatumia umeme mdogo tofauti na zilivyo zingine, ambapo mteja anaweza kuitumia katika eneo lolote.

“Tumeamua kuzindua bidhaa hii mpya kwa ajili ya kutoa fursa wa watumiaji kutopata shida katika kipindi umeme unapokatika kwani kuna sehemu ambayo inaweza kuendelea kuhifadhi vyakula kwa muda wa masaa 7 na nyingine masaa 10 bila kuharibika,” alisema.


No comments:

Post a Comment