Friday, March 7, 2014

WAFUGAJI WA TARIME WATAKA VIWANDA VYA MAZAO YA MIFUGO





Tarime. Wafugaji katika Kijiji cha Matongo-Nyamongo wilayani hapa wameiomba Serikali kufufua viwanda vya maziwa, ngozi na kuanzisha viwanda vya kusindika nyama ili kumkomboa mfugaji kimaendeleo kwa madai kuwa kukosekana kwa viwanda hivyo kunapelekea mifugo kuuzwa Kenya.

Wafugaji hao walisema, kuwapo kwa viwanda hivyo mkoani Mara kumesaidia kupata uhakika wa soko la bidhaa zao zinazotokana na mifugo na hivyo kupata faida na maisha yao kusonga mbele kwa kuwa watapata pesa na kujiletea maendeleo.

Wakiongea na gazeti hili kwa nyakati tofauti, wafugaji hao walisema kuwa, licha ya kumiliki mifugo mingi lakini hawaoni manufaa yake kwani kwa sasa lita moja ya maziwa wanauza kwa Sh1000 kutoka kwa mnunuzi mmoja mmoja pindi anapohitaji.



Lazack Kesongo mmoja wa wafugaji hao wa ng’ombe,alisema mifugo waliyonayo haiwasaidii katika kutatua matatizo yao ya kifamilia na kwamba kuisihi Serikali kuliangalia kwa umakini ombi hilo la kujengwa kiwanda cha ngozi.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele ameunga maoni hayo ya wafugaji na kusema kuwa kuna haja kweli ya Serikali na wawekezaji kufufua viwanda vya maziwa hususani mkoani Mara kwa madai kuwa kuna viwanda vingi vya maziwa ambavyo havifanyi kazi kutokana na kukosa watu wa kuzalisha.

Henjewele alisema, kutokuwapo kwa viwanda Tarime vya maziwa, ngozi na kusindika nyama, wafugaji wamekosa maendeleo na kwa sababu hiyo wafugaji hao huuza mifugo yao Kenya kwa kuwa huko kuna viwanda.

Kaimu Ofisa Mifugo, Juma Mganga alisema kuwa halmashauri ina mpango wa kuanzisha vituo vidogo vya kuuzia maziwa ambapo watu watapeleka kuuza maziwa yao na mnunuzi atafuata maziwa kwenye vituo vilivyopangwa kikiwamo Kituo cha Komaswa, Kata ya Manga ambacho kimeshaandaliwa kwa ajili ya uuzaji maziwa.

No comments:

Post a Comment