Thursday, March 6, 2014

WAFANYABIASHARA JIJINI MBEYA WASEMA MADAI YAO YA KIMSINGI




WAFANYABIASHARA Jijini Mbeya wamesema madai yao ya kimsingi si kuzigomea mashine za kielektroniki za (EFDs) wala kugoma kulipa kodi bali ni kuitaka serikali kubadilisha mfumo mzima wa ulipaji kodi.
Hayo yamesemwa jana wakati wa kutoa tamko la msimamo wa wafanyabiashara kuhusu matumizi ya mashine za risiti za kielektroniki za EFDs na Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara jijini hapa, Johnson Ntupah wakati wa mkutano huo.
Alisema kuwa kwani hata wao hawapendezwi na uwepo wa utofauti huo kati ya mamlaka husika na TRA wanatambua suala la ulipaji kodi ni suala la kisheria.
Alisema kumekuwepo na upotoshaji mkubwa tangu uanze mgogoro wa wafanyabiashara na TRA kuwa wafanyabiashara hao wamegoma kulipa kodi na kununua mashine hizo za EFDs jambo ambalo si kweli .
Aidha Katibu huyo alisema ni vyema TRA ikatoa taarifa sahihi kwa serikali badala ya kuendelea kupotosha na kutoa taarifa ambazo kimsingi si za kweli na hazilengi kuleta suluhisho la mgongano huo.
Wamedai kuwa kumekuwepo na utitiri mkubwa sana wa kodi ambapo halmashauri inazo sheria zake za ukusanyaji ushuru, Serikali Kuu, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), huku TRA ikija na sheria zake za leseni mbali na mashine hizo hivyo mfanyabiashara hujikuta akiwa katika wakati mgumu wa kuendesha biashara yake.
Akizungumza katika kikao mjumbe wa jumuiya hiyo, Boniventura mwalongo alisema si kama wafanyabiashara hawataki kutumia mashine za kielektroniki bali tatizo ni mfumo uliopo ambao ukirekebishwa wapo tayari.
Hata hivyo Mwalongo alisema serikali imekuwa na mfumo mbovu wa ukusanyaji tozo kwa wafanyabiashara hali inayosababisha wahusika kukata tamaa huku wengine wakiamua kuachana na shughuli za biashara.
Katibu huyo alisema kutokana na hali hiyo ni vyema serikali ikaliona tatizo hilo na kutafuta njia mbadala itakayosaidia kumpunguzia mzigo mfanyabiashara ili naye aweze kupiga hatua za kimaendeleo mbele tofauti na hali ilivyo sasa ambapo fedha nyingi zimekuwa zikipotea kwenye mikono ya serikali.
Hata hivyo wafanyabiashara hao wameiomba Halmashauri ya Jiji la Mbeya kupunguza utitiri wa ada za leseni na ushuru ikiwemo na kuweka katika kundi moja huku wakiruhusu kulipa  kwa awamu sanjari na kuweka utaratibu wa kukutana na wafanyabiashara mapema kabla ya kutoa maamuzi yeyote.
Wakati huo huo  Wafanyabiashara Jijini hapa wamekionya chama cha Wafanyabiashara, viwanda na kilimo (TCCIA) kuacha kuingilia masuala ya wafanyabiashara wa kati na wadogo.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Charles Syonga ambapo alisema kuwa TCCIA wamekuwa wakijiingiza katika madai yao na kutoa matamko yanayoonesha kuwa wafanyabiashara wote wametamka jambo ambalo amedai si kweli.
Hata hivyo alisema hivi karibuni TCCIA wametoa tamko la kukubaliana na gharama za mashine hizo baada ya kushiriki katika kikao na Naibu Waziri wa Fedha,Mwigulu Nchemba hivi karibuni katika ofisi za TRA Mbeya jambo ambalo amedai sio tamko la wafanyabiashara wa kati na wadogo.

No comments:

Post a Comment