Thursday, March 13, 2014

KIBAHA VIJIJINI YATENGA MILIONI 15/- KWA VIKUNDI




HALMASHAURI ya Wilaya ya Kibaha Vijijini, mkoani Pwani, imetenga sh. milioni 15 kwa ajili ya vikundi mbalimbali vya ujasiriamali.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Bi. Tatu Selemani, aliyasema hayo hivi karibuni katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kiwilaya iliadhimishwa kwenye Kijiji cha Mwanabwito, Kata ya Kikongo. 




Alisema wanawake wanapaswa kutambua kuwa, halmashauri hiyo ipo katika mikakati ya kuwaendeleza pamoja na vikundi mbalimbali vya wajasiriamali hivyo wachangamkie fursa hiyo.

"Halmashauri imetenga fedha hizi ambazo zipo, kilichobaki ni vikundi kuchangamkia fursa hii wakope na kurejesha ili ikopeshwe kwa vikundi vingine...jambo la msingi mnapaswa kuzitumia kwa shughuli za maendeleo si vinginevyo," alisema Bi.Selemani.

Kwa upande wake, mgeni rasmi ambaye alikuwa Diwani wa kata hiyo, Bi.Fatma Ngozi, aliwataka wanawake kujiendeleza kwenye vikundi ambavyo ndio mkombozi wao kwani wanapata fursa ya kukopeshana fedha ili kufanyia mambo ya maendeleo .

Kwa upande wao, mwakilishi wa wanamtandao katika kata hiyo, Bi.Mwajuma Hussein, alisema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya kukosa mikopo, mafunzo na nyinginezo.

Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii wilayani humo, Bi.Grace Msami, aliwataka wanawake kujiunga kwenye vikundi waweze kujikomboa kiuchumi na kujiletea maendeleo.

No comments:

Post a Comment