Thursday, March 13, 2014

SINGIDA KUZALISHA MAZAO TANI MIL. 1.3



MKOA wa Singida, unakusudia kuzalisha zaidi ya milioni 1.3 za mazao katika msimu wa kilimo mwaka 2013/14 ambazo zitatosheleza kwa chakula na mapato kwa wananchi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mshauri wa Kilimo mkoani humo, Bw. Lukas Mkuki, alisema mwaka 2012/13, Mkoa huo ulizalisha tani 859,544 za mazao ya chakula na tani 292,029 mazao ya biashara.

Alisema katika msimu wa kilimo 2012/13, Mkoa huo ulijiwekea lengo la kulima hekta 683,006 za mazao ya chakula zilizotarajiwa kuzalisha tani 1,045,470 na mazao ya biashara hekta 260,868 zilizopaswa kuzalisha tani 405,199. 

 "Bahati mbaya, hekta zilizotarajiwa kulimwa hazikulimwa zote kama mkoa ulivyotarajia...hadi kufikia Juni 2013, hekta 572,338 za mazao ya chakula zililimwa na hekta 206,518.2 za mazao ya biashara zililimwa.

"Hadi Agosti 2013, tani 859,544 za mazao ya chakula zilizovunwa pamoja na tani 292,029 za mazao ya biashara, kutokana na sensa ya idadi ya watu na makazi mwaka 2012, mkoa unakadiriwa kuwa na watu 1,369,034 na mahitaji ya chakula ni tani 369,639 hivyo ziada ni tani 491,480," alisema.

Aliongeza kuwa, pamoja na mkoa huo kuwa na ziada ya chakula, tathmini iliyofanyika Mei 2013 inaonyesha baadhi ya maeneo yaliyopata mvua kidogo yalitarajiwa kuwa na upungufu wa chakula kuanzia Disemba 2013 hadi Machi mwaka huu.

Katika msimu wa kilimo 2013/14, Mkoa huo umeweka kipaumbele cha mazao ya chakula kuwa ni mtama, uwele, viazi vitamu, mihogo na mikunde.

Mazao ya biashara ni alizeti, vitunguu, pamba na asali ambapo
lengo ni kulima hekta 683,006 za mazao ya chakula zinazotarajiwa kuzalisha tani 902,521 na hekta 260,868, mazao ya biashara ili kuzalisha tani 343,601.
 


No comments:

Post a Comment