JUMLA ya wakulima 600 katika Wilaya ya Kondoa
mkoani Dodoma, wamejisajili kwenye Kampuni ya Usambazaji wa Pembejeo za Kilimo
ya Farm Green Implements Tanzania Limited ili kupewa mikopo ya matrekta madogo,
maarufu kama power tiller.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni
hiyo, Othman Dunga juzi, alipokuwa akitoa maelezo ya utoaji wa mikopo ya power
tiller wilayani humo kwa Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Omar Kwaang’ aliyemwakilisha
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk Mary Nagu.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika
Kijiji cha Pahi wilayani Kondoa, Dunga alisema idadi hiyo ya wakulima 600
wanaohitaji mikopo ya matrekta hayo madogo ni ya awamu ya pili ya utoaji wa
mikopo hiyo.
Alisema kwa msimu huu wa kilimo wa 2013/2014,
kampuni hiyo imeingiza nchini zaidi ya power tiller 70 zenye thamani ya Sh
milioni 315 katika Wilaya ya Kondoa, ambapo wakulima wameweza kulima kwa wakati
na kwa muda mfupi tofauti na kilimo cha kutumia jembe la mkono au wanyama kazi.
Pamoja na kuwasaidia katika kilimo, power tiller
imewawezesha wakulima kubeba mizigo mashambani baada ya mavuno. Pia zimekuwa
zinawasaidia katika kubeba mahindi, kusaga nafaka na kumwagilia maji katika
bustani na mashamba madogo,” alisema.
Kuhusiana na waombaji hao wapya wa mikopo, Dunga
alisema kampuni hiyo inaandaa utaratibu, utakaowawezesha kupata matrekta hayo
madogo haraka ili kuwawezesha kutimiza ndoto zao za kuondokana na kilimo cha
jembe la mkono na kukuza pato lao kutokana na kuingia kwenye kilimo chenye
tija.
Kampuni inawaahidi wakulima kuwa itakuwa bega kwa
bega nao kwani kilimo ndiyo mhimili wa uchumi katika Taifa,” alisema Dunga.
Kwa upande wake, Kwaang’ alisema kampuni hiyo
imekuwa mkombozi kwa wakulima kutokana na kujibu kwa vitendo maombi ya wakulima
katika kuwapa pembejeo na zana za kisasa za kilimo kila wanapopokea maombi hayo
na kwa wakati.
Mbali ya Kondoa, tayari kampuni hiyo ya Farm Green
imesambaza matrekta madogo ya power tiller katika Wilaya za Kiteto, Manyoni,
Nkasi, Kahama, Chato, Kwimba, Mtwara Mjini na Iramba, ambapo wakulima wameweza
kubadili aina yao ya kilimo na kuingia katika kilimo chenye tija.
No comments:
Post a Comment