NMB imepongezwa
kwa kuwa benki ya mfano kwa kuwawezesha wajasiriamali, kukopa pikipiki kwa
kuchangia asilimia 30 kama malipo ya awali, kiasi ambacho Watanzania wengi
wanaweza.
Pongezi hizo
zimetolewa jana na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu(Uwekezaji na
Uwezeshaji), Dk Mary Nagu wakati akizindua mradi wa ukopeshaji wa bajaj na
pikipiki, unaotolewa na benki ya NMB.
Dk Nagu alitoa
mwito kwa benki na taasisi za fedha nchini, kubadili fikra na mtazamo wa utoaji
wa mikopo, ambao utawawezesha Watanzania wengi zaidi kukopa na kufanya
biashara.
Alisema utaratibu
wa kung’ang’ania dhamana ya mali zisizohamishika katika utoaji wa mikopo, umepitwa
na wakati.
“Taasisi za fedha
nchini inabidi zibuni njia mbadala kama ilivyofanya NMB za kutoa mikopo kwa
wananchi wengi zaidi bila kutumia dhamana ya mali zisizohamishika na endapo
watafanya hivyo watakuwa wanajenga uwezo wa wananchi kuweka amana kwenye benki
zao,” alisema.
Alisema changamoto
kubwa inayowakabili wajasiriamali nchini ni ukosefu wa mitaji, masharti magumu
ya benki na riba kubwa. Hata hivyo, Dk Nagu aliwashauri wakopaji wa vyombo
hivyo vya usafiri, kukatia bima ili tatizo likitokea wasirudi nyuma zaidi
kiuchumi kwani watatakiwa kuendelea kurejesha mikopo.
Aidha, alitoa rai
kwa madereva wa bodaboda, ambao wengi wao ni vijana, kuzingatia sheria za
usalama barabarani ili wasipunguze mapato yao kwa tozo mbalimbali, wanapovunja
sheria.
Kwa upande wake,
Mkuu wa Kitengo cha Biashara za kibenki wa NMB, Filbert Mponzi alisema mikopo
hiyo imebuniwa baada ya kuona changamoto kubwa ya ajira kwa vijana hapa nchini.
Alisema mikopo
hiyo ilianzishwa mwaka jana mkoani Dar es Salaam na baada ya kuona inakubalika
wameongeza kasi ya kuipeleka mikoa mingine.
Alisema marejesho
hufanyika katika kipindi cha miezi 24 na kwamba ili kumlinda mteja, mikopo hiyo
imewekewa bima kwa ajili ya ulemavu na kifo kitakachomtokea mmiliki wa pikipiki
iliyochukuliwa mkopo.
No comments:
Post a Comment