WAJASIRIAMALI WAUNGANA ILI KUTUNISHA MFUKO
WAJASIRIAMALI waliopo kwenye vikundi saba
tofauti vya Kuweka na Kukopa ndani ya Kijiji cha Kidogozero Wilaya ya Bagamoyo
Mkoa wa Pwani wameungana na kuwa na kikundi kimoja chenye nguvu kiitwacho
Tukishirikiana Tunaweza.
Akizungumza mbele ya wanavikundi hao pamoja na maofisa kutoka Plan
International Bi.Jema Helman na Bw.Kulwa Daud wa UHIKI, Mwenyekiti wa kijiji
cha Kidogozero, Ally Mmanga alisema kuwa hatua hiyo inalengo la kupata kikundi
kimoja chenye nguvu ambacho kitakuwa na uwezo wa kupata mikopo kutoka kwa
mashirika mbalimbali ili kujiinua zaidi kiuchumi.
Mmanga amevitaja vikundi ambavyo vimeungana kuwa ni Vijana Jembe, Wanawake
Tunaweza, Juhudi, Jitihada, Mshikamano, Jikomboe na Maskini Tunaweza umoja
ambao unajumuisha wanachama wapatao 218.
"Sisi viongozi waserikali kwanza tulikaa na viongozi wa vikundi hivi saba
na kuwafikishia mawazo yetu ya kuwataka waungane kwa lengo la kupata kikundi
kimoja chenye nguvu, tunashukuru wazo letu wakalikubali walipokwenda kuzungumza
na wenzao wakafikia maamuzi na hii leo tutapata viongozi wa muda ambao
watauongoza umoja huo," alisema Mmanga.
Alisema kwamba lengo pia ni kutunisha mfuko wa muungano wao ili waweze
kukopeshana kwa masharti nafuu, kupata pembejeo pamoja na zana za kilimo kama
trekta ili kurahisisha kilimo kwa wajasiriamali hao.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Bi. Zakia Digoo alisema kuwa
hatua hiyo inaunga mkono juhudi za serikali ambayo inawataka wananchi kujiunga
kwenye vikundi kwa lengo la kuwafikia kwa urahisi zaidi kupitia mikopo
mbalimbali.
Kwa upande wao maofisa hao kutoka Plan na UHIKU wamewataka viongozi hao
kuhakikisha wanawasiliana na ofisi hizo kwa ushauri ili malengo yao yaweze kuwa
na mafanikio na kwamba watakuwa karibu nao kufanikisha malengo yaliyowekwa na
umoja huo.
Baada ya mkutano huo wana-umoja hao waliteua viongozi ambao watawaongoza katika
kipindi hiki ambapo Mwenyekiti ni Said Sango, Ramadhani Kibambe Katibu huku
Mhazini akiteuliwa Nuru Lichapwike.
Akitoa shukrani kwa niaba ya umoja huo mwanachama Shaha Kiwilima alianza kwa
kutoa shukrani kwa serikali ya kijiji pamoja na wataalamu hao na kueleza kwamba
watajipanga kikamilifu ili kuona malengo yao yanakuwa na mafanikio.
No comments:
Post a Comment