Friday, March 14, 2014

WAKUU WA IDARA SIMAMIENI MIRADI- GAMBO





MKUU wa Wilaya ya Korogwe, Mrisho Gambo amesema Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) sio mfadhili bali ni idara ya Serikali inayojitegemea ambayo imeamua kuisaidia jamii kupambana na umaskini kwa kusaidia miradi ya maendeleo na huduma za jamii.

Alisema kuwa sio busara kwa baadhi ya wakuu wa idara na wataalamu kwenye wilaya tano zinazozunguka Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi za Korogwe, Lushoto, Mkinga, Same na Mwanga kutaka kulipwa posho na shirika hilo wakati wa usimamiaji wa miradi hiyo.

Aliyasema hayo juzi wakati akifungua warsha ya siku moja ya ujirani mwema kwa viongozi wa wilaya hizo tano wakiwemo wenyeviti wa halmashauri, maofisa tarafa, madiwani, watendaji kata na wadau wengine iliyofanyika mjini Korogwe.

Gambo alisema inashangaza wakati TANAPA ikitoa misaada kwa jamii kwa ajili ya miradi ya maendeleo na huduma za jamii, badala ya wataalamu wa halmashauri kuunga mkono jitihada hizo wanataka wapewe kwanza posho ndiyo waende kusimamia miradi hiyo.

“TANAPA huwa wanatoa msaada kama wa kujenga zahanati, shule na huduma za maji kwenye maeneo magumu kabisa. Tena wanatoa asilimia 70 ya msaada huo na jamii ichangie 30, lakini badala ya kuunga mkono jitihada hizo, wakuu wa idara ambao ndiyo wataalamu wetu wanataka kwanza wapewe posho.

“Unataka posho ya nini wakati wewe ni sehemu ya watumishi wa halmashauri na ukumbuke kitendo chako cha kutaka posho kinakwamisha mradi husika, hivyo nawaomba wataalamu wetu waache mtindo huo ambao unakatisha tamaa watu walioamua kuisaidia jamii yetu,” alisema Gambo.

Gambo aliwaomba TANAPA kujenga kituo cha polisi Kijiji cha Kalalani, Kata ya Mashewa wilayani Korogwe, kwani kitasaidia ulinzi kutokana na kijiji hicho ambacho kinajishughulisha na uchimbaji madini kuwa mpakani mwa Kenya na Tanzania.

Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Mkomazi, Donat Mnyagatwa alisema hifadhi hiyo ina miaka sita tangu ipandishwe hadhi kutoka Pori la Akiba na imeweza kupiga hatua ikiwa ni pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama eneo zima la hifadhi ikiwemo rasilimali zake zote. 

“Pia tumeboresha miundombinu na huduma kwa wageni, kujenga mahusiano mema na wananchi wa vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo, baadhi ya viongozi wa tarafa, kata, vijiji na raia wema wametoa taarifa za uhalifu ambazo zimesaidia kukamatwa majangili na kuzuia uhalifu,” alisema Mnyagatwa.





No comments:

Post a Comment