Thursday, March 13, 2014

WAZIRI ATANGAZA VITA NA WAUZA NYAMA, MACHINJIO




Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani ametangaza vita na wafanyabiashara wa maduka ya nyama ambao wamekuwa wakichinja mifugo bila ya kufuata utaratibu na kuahidi kufunga biashara zao milele.
 
Dk Kamani alitoa kauli hiyo jana alipofanya ziara ya kushtukiza katika machinjio ya kisasa ya mjini hapa ambako aliridhishwa na hali ya mpangilio wa machinjio hayo na kusema hakuna sababu ya kupeleka mifugo maeneo mengine.

Machinjio hayo yanamilikiwa kwa ubia wa Serikali na wawekezaji ambapo yana uwezo wa kuchinja ng’ombe 300 kwa siku,lakini wanachinja wastani wa ng’ombe 110 huku wakichinja mbuzi 1000 badala ya 1200.


Taarifa iliyotolewa na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Nyama Tanzania ambayo ndiyo inayosimamia machinjio hayo, Leo Akonaay ilieleza uwapo wa machinjio ambayo yapo nje ya mfumo rasmi na kwamba kwa sehemu kubwa yanasimamiwa na baadhi ya watumishi wa Serikali.

Akonaay alisema,machinjio ambayo hayapo kisheria,mengi yamekuwa yakichinja mifugo a inayosadikiwa ni ya wizi ambayo hununuliwa kwa bei ya chini.

“Ninaagiza kuanzia sasa kuwa, vita ya kuwasaka watu hao isiwe ni ya mtu mmoja wala idara, nitazungumza na wenzetu wa Mambo ya Ndani, Wizara ya Afya na uongozi wa Mkoa wa Dodoma ili tuweze kusaidiana katika mapambano hayo,” alisema Kamani.

Waziri huyo alisema, nyama ambazo zimekuwa zikiingizwa buchani baadhi huchanganywa na zile ambazo zimetoka katika machinjio rasmi ili kuwahadaa wateja.
Kuhusu soko alisema ubora wa nyama zinazotoka katika machinjio hayo zinakidhi lakini tatizo ni upatikanaji wa mifugo ya kutosha.

Pia Waziri alikubali ombi la kupitia upya sheria zinazozuia kuchinja mbuzi wenye uwezo wa kuzaa, hali inayowafanya wafugaji kuuza mifugo hiyo Kenya .

 

 

 


No comments:

Post a Comment