Wednesday, March 12, 2014

(TAHARIRI) BEI ZA PEMBEJEO SASA ZIDHIBITIWE





MAZAO ya kilimo yana mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania na yanamgusa karibu kila mwananchi, kuanzia vijijini mpaka mijini.

Ndio maana mabadiliko kidogo tu ya bei ya mazao hayo, huathiri zaidi kipato cha watu wengi mijini na hata vijijini na kusababisha mfumuko wa bei wa bidhaa zingine muhimu.

Tayari ripoti mbalimbali za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), zimeonesha kuwa kupanda kwa bei za vyakula, imekuwa mwiba mkali katika kipato cha wananchi na husababisha bei za huduma na bidhaa zingine kupanda.

Hata benki zetu zimekuwa zikirekebisha viwango vya riba kuwa vya juu, kwa madai kuwa thamani ya Shilingi ya Tanzania haiaminiki na kuongezeka kwa mfumuko wa bei, kunapunguza faida ya kuwekeza amana.

Gharama zinazosababishwa na ongezeko la riba, zimekuwa zikiathiri zaidi biashara katika sekta nyingine zote nchini kwa kuongeza gharama za biashara na hivyo kupanda zaidi kwa bei na kusababisha maisha ya wananchi kuwa magumu bila sababu za msingi.

Kutokana na athari hizi katika uchumi zinazotokana na sekta ya kilimo, tunashauri mamlaka mbalimbali zinazoshughulikia bei za pembejeo za kilimo, kuwa makini na bei hizo.

Tunasema hivyo kwa kuwa bei za pembejeo zina mchango mkubwa katika gharama za uzalishaji wa mazao ya kilimo, na ongezeko kidogo la bei hizo, huongeza gharama za uzalishaji kwa mkulima na kumlazimisha mkulima kupandisha bei za bidhaa zake na kuathiri uchumi wa Taifa.

Ndio maana hatutaacha kuunga mkono juhudi zozote za kupunguza bei za pembejeo, ikiwemo kauli ya Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, OmaryKwaang’,aliyetaka kampuni zinazokopesha matrekta, kuepuka kutoa riba kubwa.Alizema hayo juzi alipokuwa akikabidhi wakulima wa Kijiji cha Pahi matrekta madogo aina ya power tiller 70, zilizokopeshwa kwao.

Alitaka kampuni iliyotoa mkopo huo, kupunguza riba kwa kuwa vifaa hivyo tayari vimeondolewa kodi na Serikali lengo likiwa hilo hilo la kumpunguzia mkulima gharama za uzalishaji.

Umefika wakati kuwe na taasisi au mamlaka itakayowezesha kutazama kwa undani gharama za pembejeo za kilimo ili zidhibitiwe na kunusuru uchumi wetu na gharama za maisha kwa wananchi wetu.

Tunaamini inawezekana kwa kuwa mafanikio yameonekana katika sekta za maji, nishati na usafirishaji ambako wananchi walikuwa wakinyonywa mpaka taasisi za udhibiti zilipoanza kazi.

Hatuoni sababu za kushindwa kudhibiti bei za pembejeo, kwa kuwa kwanza hatua mbadala ya pembejeo, kama tunataka kuwa na mazao ya kutosha ya kilimo wakati huu wa mabadiliko ya hali ya hewa.

Lakini pia kama tulivyokwishaeleza kuwa nyongeza ya bei hizi za pembejeo, ina athari kubwa kuanzia kwa maisha ya mwananchi mmoja mmoja, kwa kuwa inagusa hitaji la lazima la kila mtu ambalo ni chakula.


Mbaya zaidi, kutokana na umuhimu wa chakula kwa kila mtu, mabadiliko kidogo ya bei katika bidhaa hiyo ya lazima kwa kila Mtanzania, yamekuwa yakitikisa mfumuko wa bei na kuathiri sekta ya benki ambazo ndiyo moyo wa mfumo wa uchumi wa soko huria tulionao.

 




No comments:

Post a Comment