WADAU wanaoshughulika moja kwa moja na mchakato wa
usajili wa kampuni hapa nchini, wametakiwa kufanya kazi kwa karibu zaidi ili
kuimarisha kiwango cha Tanzania kimataifa katika kujenga mazingira ya biashara.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk Florens
Turuka amesema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa CEO
Roundtable.
Alifafanua kuwa mamlaka hizo zinatakiwa kutekeleza
mradi unaojulikana kama Tanzania Investment Window Project kabla ya Mei mwaka
huu ili faida za ubunifu wake uunganishwe katika viwango vya mwaka kesho
vinavyohusu jinsi nchi zinavyoimarisha mazingira ya biashara.
Mradi huo unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa
Mataifa la Maendeleo (UNDP) na mpango wa ONE UN, unalenga kuwezesha kampuni za
ndani na za nje kujisajili kwa urahisi zaidi na kwa muda mfupi.
Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) kwa msaada wa
kiufundi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa Linalohusika na Biashara na
Maendeleo (UNCTAD) liko katika juhudi kuhakikisha kuwa taratibu za usajili wa
kampuni unarahisishwa kupitia mtandao.
Mpango huo uliasisiwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
mwezi Oktoba mwaka jana nchini China.
Mpango huo utaruhusu wawekezaji kusajili kampuni,
kupata vibali vya uwekezaji, vibali vya kazi na huduma nyingine kupitia njia ya
mtandao.
Dk Turuka alitaja baadhi ya taasisi zinazotakiwa
kufanya kazi kwa karibu kama Wakala wa Usajili wa Makampuni (Brela), Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), Wizara ya Biashara, Mamlaka ya Mifuko ya Hifadhi ya
Jamii (SSRA), Jiji la Dar es Salaam na TIC.
No comments:
Post a Comment