Tuesday, March 11, 2014

WAJASIRIAMALI WANUFAIKA SOKO LA HISA



KATIKA jitihada za kutatua changamoto za mitaji nchini kwa wajasiriamali wadogo na wa kati, soko la hisa la Dar es Salaam limeanzisha soko la kukuza ujasiriamali ambalo litawahudumia wajasiriamali wadogo na wale wa kati katika kurahisisha upatikanaji wa mitaji wanayohitaji.

Ameyasema hayo Bw. Emmanuel Nyalali kutoka Soko la Hisa la Dar es Salaam (EGM) wakati akizungumza na wadau wa biashara wilayani Babati mkoani Manyara katika semina ya soko la kukuza ujasiriamali, ambapo amedai kwamba soko la kukuza ujasiriamali yaani (EGM) linatoa suluhu kwa changamoto zinazowakabili wajasiriamali katika upatikanaji wa uhakika wa mitaji ya muda mrefu kwa ajili ya kuendeleza biashara zao. 

Aidha, Nyalali alisema kwamba makampuni madogo na ya kati (SMEs) mengi yanayofanya biashara hayana mazoea ya kuweka vizuri rekodi za biashara zao na hiyo huleta changamoto katika kufanya makadirio ya mitaji na mauzo.

Pia alisema kwamba changamoto kuu zinazokwaza maendeleo ya makampuni madogo na kati (SMEs) ni kutokuwepo kwa mazingira mazuri ya kibiashara, ukosefu wa ujuzi katika uendeshaji na usimamizi wa biashara pamoja na ukosefu wa upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya ukuzaji wa biashara.

Awali, akifungua semina ya wadau hao,Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Bw. Elastol Mbwilo alilitaka soko la hisa kuhakikisha linatoa elimu ya kutosha hadi ngazi ya chini badala ya kutoa elimu kwa wafanyabiashara wakubwa pekee ili wapate kutambua umuhimu wa soko la hisa ambalo litasaidia kubadilisha uchumi wao kwa haraka.


No comments:

Post a Comment