Sunday, March 9, 2014

SEKONDARI YAANZA KUFUNDISHA UJASIRIAMALI




SHULE ya Sekondari ya Winning Spirit iliyopo jijini Arusha, imekuwa ya kwanza, kufundisha somo la ujasiriamali kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi kujiajiri pindi wanapohitimu masomo yao na kuepukana na changamoto za ajira inayoikabili taifa. 

Aidha wito umetolewa kwa shule zingine nchini kuingiza mitaala hiyo shuleni ili kusaidia wanafunzi kujiajiri na kuondokana na wimbi la vijana wengi wanaohitimu vyuo kukosa ajira na hivyo kuchangia ukosefu wa ajira kuendelea kuongezeka.

 Akizungumza na wazazi, walezi pamoja na wanafunzi katika mahafali ya tano ya kidato cha nne ya shule hiyo Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Mkoa wa Arusha, Bw. Nicholous Duhia alisema kuna umuhimu mkubwa kwa shule mbalimbali hapa nchini kuanza kuingiza mitaala ya ujasiriamali. 

Alisema kuwa ili kuwawezesha wanafunzi kupata elimu ya ujasiriamali wakiwa na umri mdogo na kuondoa changamoto kubwa iliyopo ya wanafunzi wengi kutopata ajira pindi wanapohitimu masomo yao ni bora utaratibu huo utasaidia kupuguza tatizo hilo. 

"Kwa kweli naipongeza shule hii kuwa ya kwanza kuanzisha mtaala wa ujasiriamali katika masomo yao, kwani wataweza kuwasaidia wanafunzi wengi kujiajiri na kutoishia kukaa majumbani baada ya kuhitimu masomo yao kutokana na kutokuwa na kazi za kufanya, hivyo mfano huu unapaswa kuigwa na shule mbalimbali kwani ni utaratibu mzuri sana,"alisema Bw. Duhia.



 Naye Mkurugenzi wa shule hiyo, Bw. Maximilian Iranghe alisema kuwa, shule hiyo imefikia hatua ya kuanzisha somo hilo shuleni hapo baada ya kuona wanafunzi wengi wamekuwa wakihitimu masomo yao na kukosa ajira na hivyo kuendelea kuongeza idadi ya vijana wasiokuwa na ajira nchini.
Alisema shule hiyo imekuwa ikishirikiana na Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogovidogo (SIDO) kwa lengo ya kufundisha elimu hiyo ambapo wanafunzi wengi wamependa somo hilo litakalowasaidia katika maisha yao. 

"Sisi tumeamua kuanzisha masomo haya ya ujasiriamali na ufundi stadi kwa shule yetu kwani tumegundua kuwa sio wanafunzi wote ambao wanaweza kupata alama nzuri na kuweza kuendelea na elimu ya juu, hivyo kwa wale ambao hawataweza kuendelea na elimu hiyo wataweza kujiajiri wenyewe badala ya kukaa majumbani bila kazi,"alisema Iraghe. 

Aidha aliwataka wanafunzi hao kutobweteka kwa elimu ya kidato cha nne waliyoipata shuleni hapo badala yake wajiendeleze zaidi kwa ajili ya maisha yao ya baadaye ili waweze kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanayobadilika mara kwa mara.  

No comments:

Post a Comment